RAIS Dk Samia Suluhu Hassan ni kichecheo kwa wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Lumumba kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Mussa Hassan Mussa, ameyasema hayo wakati akizungumza na Nipashe Digital, mwishoni mwa wiki, akiwa Ofisini kwake shuleni hapo Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema watoto wa kike wamehamasika kusoma na ufaulu wao ni mzuri zaidi ikilinganishwa na wanaume kutokana na hamasa ya uwepo wa Rais mwanamke, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumzia ufaulu wa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, amesema ubora wa matokeo na ufaulu ni mzuri ambapo shule hiyo imetoa ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi 75, daraja la pili 84 na daraja la tatu 18 kati ya wanafunzi wote 177 waliofanya mitihani hiyo na kwa matokeo ya kidato cha nne wanafunzi wote walipata daraja la kwanza na kati ya wanafunzi hao 177 wasichana walikuwa 87 na wanaume 90.
“Tunajivunia kwamba wanafunzi wote hakuna anaepata daraja sifuri wala daraja la nne na miongoni mwa siri ya mafanikio ni ushirikiano wa wazazi wa wanafunzi pamoja wa walimu wa shule hii,” anasema.
Amesema pia shule inajivunia kuwa miongoni mwa shule kongwe zilizofundisha viongozi mashuhuri akiwemo Rais wa sasa wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Mmarais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED