Miradi ya bil. 24 ya TACTIC kujengwa Singida

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 06:12 PM Jun 03 2025
Miradi ya bil. 24 ya TACTIC
 kujengwa Singida
Picha: Mpigapicha Wetu
Miradi ya bil. 24 ya TACTIC kujengwa Singida

Halmashauri ya Manispaa ya Singida imesaini mkataba na mkandarasi wa kampuni ya M/s Sihotech Engeneering Company Limited kwa ajili ya ujenzi wa miradi mitatu likiwamo soko la kimataifa la vitunguu ambayo itakapokamilika itagharimu Sh.Bilioni 24.748.

Utiaji saini huo ambao umefanyika kati ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida,Joanfaith Kataraia na Mkurugenzi wa kampuni hiyo Mhandisi Adam Sebastian na kushuhudiwa na Naibu Waziri,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego.

Miradi itakayotekelezwa katika Manispaa ya Singida kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) mbali na ujenzi wa soko la vitunguu la kimataifa mingine ni barabara za katikati ya mji zenye urefu wa kilometa 7.52 na ujenzi wa mtaro wa maji ya mvua wa Mnung'una wenye urefu wa kilometa 2.6.

Naibu Waziri TAMISEMI, Katimba akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini mkataba huo, amesema miradi hiyo ni fursa kubwa kwa wananchi wa Singida hususani wafanyabiashara wa vitunguu ambao watakwenda kunufaika na ujenzi wa soko la kimataifa la vitunguu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dendego,  amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni habari njema kwa wanasingida katika kuelekea safari ya upatikanaji wa jiji la Singida ikiwa ni matokeo ya ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa serikali, chama na wananchi wa mkoa huo.

1

Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida,  Kataraia amesema atahahakikisha anasimamia kikamilifu ujenzi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa mujibu wa makubaliano waliyoingia na kampuni hiyo.

Naye Mratibu wa miradi ya Benki ya Dunia kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Humphrey Kanyenye,amesema ujenzi wa miradi hiyo uataanza Juni 26, 2025  ambapo itatekelezwa kwa kipindi cha miezi 15.

Amesema wakandarasi wazawa wawd wanajitokeza kwa wingi kuomba tenda mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya  TACTIC ili kuweza kunufaika na fursa hiyo kama sehemu ya kukuza uchumi wa Tanzania na kuimarisha mzunguko wa fedha nchini.

Kanyenye amesema kuwa miradi hiyo ya TACTIC itakapokamilika italeta manufaa makubwa kwa Manispaa ya Singida ikiwemo kuongeza fursa za ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha hali ya biashara katika maeneo husika hivyo kuchangia maendeleo ya muda mrefu ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Soko la Kimataifa la Vitunguu litakalojengwa kata ya Misuna Manispaa ya Singida litakuwa ni jengo la ghorofa mbili likiwa na eneo la kuchambua vitunguu, kukaushia vitunguu, maduka 10, vyumba 4 vya huduma za kifedha, pamoja na maeneo mengineyo, likitarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida kutoka Sh. Milioni 300 hadi Milioni 505 litakapokamilika.

2