Wadau zaidi ya 500 wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kushiriki katika Tuzo za 32 za Kimataifa za Utalii kwa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi, zitakazofanyika nchini Tanzania tarehe 28 Juni, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 11, 2025, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, amesema uchaguzi wa Tanzania kuwa mwenyeji pekee wa hafla hiyo kwa mwaka huu ni uthibitisho wa mafanikio na hadhi inayozidi kukua ya taifa hilo katika tasnia ya utalii duniani.
“Tanzania imepewa heshima hii kubwa kutokana na mchango wake mkubwa na mafanikio yanayoonekana katika sekta ya utalii, sambamba na ushahidi wa hadhi inayozidi kupanda kimataifa,” amesema Mafuru.
Ameeleza kuwa tuzo hizo zitajumuisha taasisi na mashirika 50 kutoka Tanzania, ambapo 38 ni kutoka sekta binafsi na 12 kutoka taasisi za serikali, ambayo yote yatashindana na wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Kwa mujibu wa Mafuru, Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji sambamba na mataifa mengine makubwa katika sekta ya utalii duniani kama Mexico, Hong Kong, Italia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na Bahrain, ambayo yatakuwa wenyeji wa hafla hizo katika kanda zao.
“Tanzania ni nchi pekee Afrika kushika nafasi hii kwa mwaka huu. Hafla hii itafanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam,” amebainisha Mafuru.
Akitaja vipengele vya ushindani, amesema tuzo hizo zinaandaliwa na World Luxury Media Group, taasisi iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa lengo la kutambua mchango wa wadau muhimu katika ukuzaji wa sekta ya utalii duniani. Kwa Tanzania, amesema ni fursa adhimu kuonesha uwezo wake na vivutio lukuki ilivyonavyo.
“Washiriki watashindania tuzo katika vipengele mbalimbali vya mnyororo wa thamani wa utalii, vikiwemo hifadhi za taifa, hoteli, mashirika ya ndege, kampuni za usafirishaji na ukodishaji magari, bandari, pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA),” amefafanua.
Ameongeza kuwa vipengele vingine vitahusu ubora wa huduma mbalimbali kama malazi, usafiri wa anga, ardhini, baharini na reli, huduma za chakula, pamoja na shughuli za kitalii kama kupanda milima na safari za wanyamapori (adventure tourism).
Ili kuhakikisha wageni kutoka mataifa mbalimbali wanapata uzoefu wa kipekee na kuwa mabalozi wa utalii wa Tanzania duniani, Mafuru amesema waandaaji wameandaa safari maalum nne za mafunzo (familiarization trips) ambazo zitawapeleka washiriki kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, kujionea uzuri, urithi wa asili na ukarimu wa Watanzania.
“Tunaamini wageni hawa wataondoka wakiwa mabalozi wazuri wa Tanzania kimataifa,” amesema Mafuru.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED