Elon Musk aunga mkono wazo la Marekani kujiondoa UN na NATO

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:44 AM Mar 03 2025
Bilionea Elon Musk na Rais wa Marekani Donald Trump.
Picha: Mtandao
Bilionea Elon Musk na Rais wa Marekani Donald Trump.

Bilionea Elon Musk ameonyesha kuunga mkono wazo la Marekani kujiondoa katika Umoja wa Mataifa (UN) na Muungano wa Kijeshi wa NATO.

Akijibu chapisho la mtandaoni jana Jumapili lililohimiza hatua hiyo, Musk, ambaye anaongoza Idara ya Ufanisi wa Serikali ya Marekani (DOGE), aliandika kwa ufupi: "Ninakubaliana."

Rais wa Marekani, Donald Trump, na wabunge wa chama cha Republican wameahidi kutathmini upya ushiriki wa Washington katika UN na NATO. 

Mnamo Februari, Seneta Mike Lee wa Utah aliwasilisha mswada wa DEFUND Act, unaopendekeza Marekani ijiondoe kabisa kutoka UN. Lee alikosoa Umoja wa Mataifa kama “jukwaa la madikteta” linalopinga Marekani na washirika wake, akisema licha ya ufadhili mkubwa, UN imeshindwa kuzuia vita, mauaji ya kimbari, ukiukwaji wa haki za binadamu, na majanga ya kiafya.