Odinga awasihi CHADEMA kufanya mazungumzo na Serikali, atarajia uchaguzi wa amani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:54 AM Mar 23 2025

Odinga na viongozi hao wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu wamekutana jana Jumamosi Machi 22, 2025 nchini Kenya.
Picha: Mtandao
Odinga na viongozi hao wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu wamekutana jana Jumamosi Machi 22, 2025 nchini Kenya.

Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga kupitia mtandao wake wa Facebook amesema kuwa amewasihi viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutanguliza mazungumzo na ushirikiano wenye kujenga na Serikali.

Odinga na viongozi hao wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu wamekutana jana Jumamosi Machi 22, 2025 nchini Kenya ikiwa ni miongoni mwa kukutana na makundi mbalimbali kueleza kaulimbiu yao ya 'No Reform, No Election.'

"Nilifanya mazungumzo na viongozi wa upinzani wa Tanzania walionitembelea. Tulibadilishana mawazo kuhusu uimarishaji wa demokrasia katika bara hili, ikiwa ni pamoja na mchango madhubuti katika maendeleo ya taifa na vyama ndani na nje ya serikali.

"Niliwahimiza kutanguliza mazungumzo na ushirikiano wenye kujenga na serikali yao kwa maslahi ya taifa na uhifadhi wa demokrasia ya Tanzania,"ameandika Odinga. Aidha, Odinga amesema anatarajia uchaguzi wa amani na uwazi nchini Tanzania. 

Kauli hiyo ameitoa wakati CHADEMA ikisitiza kuwa hakutakuwa na uchaguzi kama mabadiliko yasipofanyika.