Rais Samia Suluhu Hassan, leo Aprili 9, 2025, anatarajiwa kutembelea kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta cha Luanda Oil Refinery ikiwa ni siku ya tatu na ya mwisho ya ziara yake ya kikazi nchini Angola.
Ziara hiyo inaweka alama muhimu ya kihistoria, kwani ni mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania kutembelea rasmi Angola tangu mwaka 2006. Kabla ya hapo, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ndiye aliyekuwa kiongozi wa kwanza wa Tanzania kufanya ziara ya Kiserikali nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Sharifa Nyanga, lengo la kutembelea kiwanda hicho ni kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi na maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi, hasa kwa kuzingatia kuwa Tanzania ina hifadhi kubwa ya gesi, huku Angola ikiwa ya pili barani Afrika kwa hifadhi ya mafuta.
"Akiwa kiwandani, Mheshimiwa Rais Samia atapokelewa na Waziri wa Madini wa Angola, Mhe. Diamantino Pedro Azevedo, ambapo watajadili fursa za ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi, pamoja na namna ya kukuza uwezo wa kitaalamu katika nyanja hizo," alisema Nyanga.
Rais Samia yuko Angola kwa mwaliko wa Spika wa Bunge la Angola, Carolina Cerqueira, ambaye pia ni mwanamke, na jana alimpokea kwa heshima kubwa Bungeni. Samia ameweka historia kwa kuwa Rais wa kwanza Mwanamke kutoka Afrika kulihutubia Bunge hilo.
Ziara hii inaleta kumbukumbu ya mahusiano ya muda mrefu kati ya Tanzania na Angola na inaonesha dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kupitia ushirikiano wa kimataifa, hasa katika sekta muhimu kama mafuta na gesi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED