Trump asitisha misaada ya kijeshi kwa Ukraine kufuatia mzozo na Zelenskiy

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:42 AM Mar 04 2025
@nipashedigital #Video Rais wa Marekani Donald Trump amemtaka Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kukubali masharti ya amani na Urusi wakati wa mkutano wa pamoja uliofanyika Ikulu ya White House Marekani jana Februari 28. Trump alimtaka Zelensky kufanya makubaliano na Urusi ili kumaliza mzozo unaoendelea, akionya kuwa kutokubali kufanya hivyo kunaweza kusababisha kupoteza msaada wa Marekani. Hata hivyo, Zelensky alikataa pendekezo hilo, akisisitiza kuwa haiwezekani kufanya makubaliano na Rais wa Urusi Vladimir Putin kutokana na vitendo vya kikatili vilivyofanywa na vikosi vya Urusi nchini Ukraine. Kusoma habari hii zaidi tembelea epaper.ippmedia.com #NipasheMwangaWaJamii #NipasheDigital ♬ original sound - Nipashe Digital
Rais wa Marekani, Donald Trump.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesitisha misaada yote ya kijeshi kwa Ukraine kufuatia mzozo wake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, wiki iliyopita, kwa mujibu wa afisa wa Ikulu ya White House.

"Rais Trump amekuwa wazi kuwa anataka amani. Tunataka pia washirika wetu wajitolee kwa lengo hilo. Tunasitisha misaada yetu na kuikagua ili kuhakikisha inachangia katika suluhu," amesema afisa huyo siku ya Jumatatu, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ikulu ya White House haijafafanua aina na kiwango cha misaada itakayositishwa wala muda ambao hatua hiyo itadumu. Aidha, ofisi ya Zelenskiy haijatoa tamko lolote kupitia Ubalozi wa Ukraine huko Washington.

Hatua hii inakuja baada ya Trump kubadili msimamo wa Marekani kuhusu Ukraine na Urusi alipoingia madarakani Januari, akichukua mtazamo wa urafiki zaidi kwa Moscow.

Uamuzi huu pia unafuatia mabishano makali kati ya Trump na Zelenskiy katika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa, ambapo Trump alimlaumu Zelenskiy kwa kutothamini vya kutosha msaada wa Marekani katika vita vya Ukraine na Urusi.