Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, umetangaza kuzizuia fedha za serikali zenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 2 ($2bn) zilizokuwa zimepangwa kutolewa kwa Chuo Kikuu cha Harvard, saa chache baada ya chuo hicho kukataa kutekeleza matakwa ya Ikulu ya White House.
Katika taarifa yake, Idara ya Elimu ya Marekani ilisema:
"Taarifa ya Harvard leo inaangazia kile ambacho kimejitokeza kuwa tatizo katika vyuo na vyuo vikuu vya kitaifa."
Wiki iliyopita, Ikulu ya White House ilituma orodha ya matakwa kwa Harvard ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi katika taasisi za elimu ya juu. Miongoni mwa matakwa hayo yalikuwa ni pamoja na mabadiliko katika uongozi wa chuo, sera za ajira, na taratibu za usajili.
Harvard imekuwa chuo kikuu cha kwanza nchini Marekani kupinga hadharani shinikizo hilo kutoka kwa utawala wa Trump, likikataa kufanya mabadiliko yaliyoelekezwa ambayo yangetoa nafasi kwa serikali kuingilia kwa kiwango kikubwa shughuli za ndani za chuo hicho.
Rais Trump amevituhumu vyuo vikuu mbalimbali kwa kushindwa kuwalinda wanafunzi wa Kiyahudi, hasa katika kipindi cha maandamano makubwa yaliyofanyika katika vyuo mbalimbali nchini mwaka jana, kupinga vita vinavyoendelea huko Gaza pamoja na uungwaji mkono wa Marekani kwa Israel.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED