MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mbeya, imemhukumu Evaristo Mwakyoma (69), mkazi wa Mapelele, kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumlawiti mtoto wa jirani yake, mwenye umri wa miaka mitano.
Hukumu hiyo ilitolewa Februari 25, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Teddy Mlimba, baada ya Mwakyoma kupatikana na hatia ya kutenda kosa hilo.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 154 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Hakimu Mlimba alieleza kuwa Mwakyoma alitenda kosa hilo tarehe 18 Aprili 2024, katika eneo la Mapelele, alimdanganya mtoto huyo na kumfanya kitendo cha kikatili cha kumlawiti.
Kutokana na kitendo hicho Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa, amewataka wananchi na watu wengine wenye tabia kama ya Mwakyoma kuacha mara moja, akisisitiza kuwa vyombo vya sheria havitayafumbia macho matukio ya aina hiyo.
Kamanda Siwa, pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, ili haki ipatikane.
Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na Askari wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wamewakamata watuhumiwa wanne wakiwa na nyara za serikali bila kibali.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Isack Mahuvi (35), mkazi wa Mlonga, Joseph Mhelela (45), mkazi wa Kijiji cha Chalisuka, na Songa Kapunga (80) na Dogani Kapunga (70) wote wakazi wa Kijiji cha Igunda.
Amesema wamekamatwa wakiwa na vipande viwili vya meno ya tembo, kipande kimoja cha ngozi ya Nyati, miguu nane ya wanyama, ngozi moja, kichwa kimoja na sikio moja la swala.
Ameeleza kuwa watuhumiwa hao ni wawindaji haramu na kwamba vyombo vya sheria vitaendelea kupambana na ujangili na kuhakikisha wanashughulikia vikali wahalifu wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED