Amref Tanzania yajinasibu mafanikio ya Mradi wa Thamini Uzazi Salama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:59 AM May 06 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha (kushoto) akipewa maelezo katika banda la Amref Tanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkunga Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani humo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha (kushoto) akipewa maelezo katika banda la Amref Tanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkunga Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani humo.

Katika kuadhimisha Siku ya Mkunga Duniani kitaifa iliyofanyika mkoani Shinyanga, Shirika la Amref Health Africa Tanzania limeeleza mafanikio makubwa ya Mradi wa Thamini Uzazi Salama, unaolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa wanawake na watoto wachanga kupitia uwezeshaji wa wakunga na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Zimamoto, Meneja wa Programu ya Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana wa Amref Tanzania, Dk. Serafina Mkuwa alisema:


“Mradi huu unafadhiliwa na Global Affairs Canada (GAC) na unasimamiwa na UNFPA. Unalenga kuongeza upatikanaji wa wakunga wenye ujuzi na kuboresha huduma katika vituo vya afya, taasisi za mafunzo na kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii,” alisema Dk. Mkuwa.


Dk.Mkuwa aliongeza kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, mradi huo umefanikiwa kuwafikia watu 17,167 kupitia uhamasishaji wa afya ya uzazi, jinsia na ukatili wa kijinsia (GBV), kutoa mafunzo kwa waelimishaji rika wa kiume 142, na kuimarisha uwezo wa wasimamizi 112 wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) kupitia jukwaa la LEAP.

“Mradi pia umewezesha CHW 112 kwa kuwapatia simu za mkononi, kuwawezesha viongozi wa jamii 424 kuhusu jinsia na haki za afya ya uzazi, na kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati za usimamizi wa vituo vya afya na wakuu wa vituo 518 kuhusu bajeti na mipango ya afya,” alieleza zaidi Dk. Mkuwa.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, aliishukuru Serikali kwa kuimarisha miundombinu ya afya mkoani humo, akisema:

“Kati ya mwaka 2015/2016, asilimia 66 ya wanawake walijifungulia katika vituo vya afya. Kwa sasa idadi imeongezeka hadi asilimia 85. Hii ni hatua kubwa kuelekea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.”


Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania, Dk. Beatrice Milike, alisisitiza mchango wa wakunga nchini:

“Wakunga hutoa asilimia 90 ya huduma za afya ya uzazi nchini. Ikiwa watawezeshwa kwa mafunzo na vifaa, wanaweza kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa zaidi ya asilimia 87,” alisema Dk. Milike.


Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Mkunga ni Nguzo Muhimu katika Kila Janga”, ikionyesha umuhimu wa wakunga hasa katika nyakati za dharura kama vile majanga ya kiafya na kijamii.

Mradi wa Thamini Uzazi Salama umeendelea kuwa mfano bora wa ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kimataifa na jamii katika kuhakikisha uzazi salama na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa mama na mtoto nchini Tanzania.