MBUNGE wa Jimbo la Kishapu, Boniphace Butondo, ametoa vifaa vya TEHAMA kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Kishapu, ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, kuboresha sekta ya elimu, wanafunzi wasome na kupata ufaulu mzuri.
Amekabidhi vifaa hivyo jana, Machi 22, 2025 shuleni hapo.
Butondo akikabidhi vifaa hivyo, amesema yeye akiahidi huwa anatekeleza, aliwahidi wanafunzi hao kuwapelekea vifaa hivyo pamoja na televisheni, kwa ajili ya kuangalia taarifa ya habari hasa kwa siku za wikiendi.
“Leo nimetekeleza ahadi yangu kwenu na kuwaletea vifaa hivi vya TEHAMA, televisheni ambayo mliniomba kwa ajili ya kuangalia taarifa ya habari,” amesema Butondo.
Aidha, ameomba vifaa hivyo vitunzwe pamoja na kutumiwa vizuri, ili vidumu kwa muda mrefu, huku akiwasisitiza wanafunzi wasome kwa bidi ili watimize ndoto zao.
Diwani wa Kishapu, Joel Ndetoson, amempongeza Mbunge Butondo kwa kutekeleza ahadi zake,na kutoa vifaa hivyo vya TEHAMA shuleni hapo, huku akiahidi kumuunga mkono kwa kununua kifurushi kila mwezi, ili wanafunzi hao wawe wanaangalia taarifa ya habari na kuona mambo ya maendeleo ambayo anayafanya Rais Samia.
”Shule yetu hii imekuwa ikifanya vizuri katika taaluma na tunamshukuru Mbunge kwa kutuletea vifaa hivi vya TEHAMA, mfano kwa matokeo ya mwaka 2024 ya kidato cha nne, wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 94, daraja la kwanza walipata wanne, la pili 19, tatu 40 na daraja la 4 walikuwa 31,” amesema Buhoro.
Nao baadhi ya wanafunzi, wamemshukuru Mbunge Butondo kwa kutekeleza ahadi yake kwao, huku wakimuahidi watasoma kwa bidii.
Butondo mbali na kutoa vifaa hivyo vya TEHAMA kwa wanafunzi hao, pia aliwapatia mchele, kwa ajili ya kula chakula cha jioni na kubadilisha mlo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED