DC Lulandala awapa mchongo World Vision

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 12:30 PM Apr 30 2025
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Faki Lulandala, akikabidhi sare za shule kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Losinyai.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Faki Lulandala, akikabidhi sare za shule kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Losinyai.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, Faki Lulandala, ameapa kula sahani moja na wazazi wanaotoka jamii ya kifugaji ya Kimasai wasiotaka kuwasomesha watoto shule, wakisubiri kusaidiwa na serikali au wahisani, likiwemo Shirika la World Vision Tanzania.

Akizungumza jana na wakazi wa Kijiji cha Losinyai, Kata ya Oljoro No.5, Wilayani humo, amesema anatamani kuona World Vision Tanzania, katika eneo hilo la kusaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi, wanawafikia watoto hao wenye uhitaji, huku akielekeza wazazi wenye utajiri wa mifugo, hasa ng’ombe 700 wasisaidiwe.

Lulandala, alikwenda Kata ya Oljoro No.5 kwenye hafla ya makabidhiano ya madawati 200, sare za shule kwa wanafunzi 738, pamoja na kuzindua Mradi wa Maendeleo ya Jamii wa World Vision Tanzania, Oljoro AP.

Mradi huo wa miaka 12 ulioanza mwaka wa fedha 2024/25, unatekelezwa na World Vision Tanzania, kwa ufadhili wa Ireland.

“Nilienda Tarafa moja hapa hapa Simanjiro, akasimama mzee mmoja kasema nimekuja kwako nimekwama, naomba msaada mheshimiwa Mkuu wa Wilaya umekuja. Nikamuuliza msaada gani, akasema watoto, yaani hapa nimezidiwa nataka kupeleka watoto shule. Nikamwambia pole, sasa mimi nifanyaje, nikamuuliza una wangapi, akasema ana watoto 78.


“Nikamuuliza una ng’ombe wangapi, akasema wamekufa wameisha kabisa, wamebaki ng’ombe kama 700 tu. Anaona utajiri huo alionao bado hawezi kununua sare za watoto wa shule, hana uwezo wa kuchangia chakula cha mtoto wake shuleni, ameshafilisika tayari. Anahisi anahitaji World Vision waje wamsaidie, ni sawa kweli?
…Natamani World Vision, kwenye eneo hili la kusaidia watoto muwafikie watoto wenye uhitaji. Ukiona ana ng’ombe 700 wala huyo usimsaidie,na asipopeleka mtoto shule, wewe tutaarifu sisi kama hataki atapeleka hata kwa fimbo.”

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Oljoro No.5 wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo.

Akiwa Kata hiyo Oljoro No. 5, Mkuu huyo wa Wilaya, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kila kibao au bango la shule za Wilaya hiyo yaandikwe maandishi makubwa, ‘Elimu na Chakula ni Haki yetu, Wazazi Tulisheni’

“World Vision Tanzania wanapofanya haya, hawasemi sisi tupumzike. Tumeupokea kama kichocheo na sio ukatufanye tustarehe. Nimeambiwa miradi ambayo inatekelezwa kwa Kata ya Oljoro No 5, ina thamani ya Sh. milioni 51, si si kidogo, asanteni. Mchango au msaada ambao World Vision Tanzania mmeutoa tunaupokea kwa mikono miwili.


Aidha ameongeza: “Ni jukumu letu akija World Vision Tanzania kama ambavyo leo amekuja, amekuta tuna changamoto ya madawati yanayofikia 593, ametuletea madawati 200, anatuacha na changamoto ya 400 na zaidi. Tusiseme tunamsubiri World Vision Tanzania kutatua, kile mlichokifanya kiwe ni kichocheo cha kutufanya tutafute madawati.”

Mratibu wa Mradi wa World Vision Tanzania-Oljoro AP, Pruth Daudi, amemweleza Lulandala kwamba, shule sita za msingi za Losinyai, Endupoto, Eionot, Oljoro No. 5, Kampuni na Oiborkishu, zitanufaika na msaada huo.

Amesema msaada huo unahusisha sare za shule kwa wanafunzi 738, ambao ni watoto wanaofadhiliwa na wale wenye uhitaji wa sare, ambapo watoto 1,338 watanufaika, wakiwamo wavulana 613 na wasichana 725.

Kuhusu madawati, Peruth, amesema yanakwenda kupunguza tatizo la upungufu wa madawati katika shule za kata hiyo.

Jengo jipya la Ofisi ya Mradi wa Maendeleo ya Jamii wa Oljoro AP, ambalo litatumika kutekeleza mradi huo.