WAKAZI wa Kijiji cha Mkonko Kata Kamsamba Wilaya ya Momba mkoani Songwe, wameondokana na kero ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita nane kufuata matibabu kijiji jirani baada ya kukamilika kwa ujenzi wa zahanati.
Wakazi hao, wamejenga zahanati hiyo kwa kushirikiana na Kampuni ya Helium One inayochimba gesi kijijini hapo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe, wakazi hao wameishukuru kampuni hiyo kwa kujenga zahanati hiyo na kuokoa maisha yao hususani wajawazito.
"Nawashukuru sana Helium One kwa kutujengea zahanati, imetupunguzia kero ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za kitabibu," amesema mmoja wa wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Nkana.
Merisiana Misale, ameishukuru serikali kwa kuwapa kibali wawekezaji hao katika eneo hilo na kuwasaidia kujenga zahanati hiyo.
Misale, ameahidi wataitunza zahanati hiyo, ili idumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Muuguzi Mfawidhi wa Zahanati hiyo, Aneth Willium, amesema wamekuwa wakipokea wagonjwa wengi na kuwapatia matibabu.
Aneth, amesema wakazi wa kijiji hicho, wamekuwa mstari wa mbele kujitolea kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali na sekta binafsi.
Amesema moyo wao huo, ni mafanikio ya kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati.
Msimamizi wa Mradi wa Utafiti wa Gesi ya Helium, Emmanuel Gachocha, amesema kwa kutumia Fedha za Uwajibikaji kwa Jamii, (CSR), kwa mwaka 2021/22, walitoa Shilingi milioni 55 kuboresha na kukarabati shule za kata.
Ghachocha, amesema mwaka 2022/23 walitumia Shilingi milioni 54 kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo, ujenzi wa vyoo na vifaa vya kuchomea taka.
Amefafanua zaidi ya kuwa mwaka 2024 na wametumia shilingi milioni 20 kwa ununuzi wa vifaa tiba na dawa kwa jamii.
Amesema walitoa msaada katika Kata ya Uvuna na Itumbula kwa familia zilizokumbwa na maafa ya mvua Februari mwaka huu baada ya nyumba za kaya zaidi 15 kuharibiwa.
Ameeleza zilitumika shilingi milioni 13, kwa ajili ya kununua saruji na mabati kwa ajili ya kukarabati nyumba hizo na kiasi kingine kununua vyakula.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED