Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka huu, Ismail Ali Ussi, ameonyesha kuguswa na wanafunzi wa shule za sekondari Dk. Samia na Bunge kwa kuwasilisha ujenzi wa athari za rushwa katika Uchaguzi Mkuu nchini.
Ussi alisema anawapongeza wanafunzi hao kwa kuonyesha uwezo mkubwa katika kujadili rushwa kwenye uchaguzi katika mdahalo wao.
Alisema uwezo wa mada walizojadili wanafunzi hao kwenye mdahalo huo, inaonyesha jins Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inavyoelimishha vijana hao kuhusu madhara ya rushwa katika sekta mbalimbali nchini.
"Naipongeza sana TAKUKURU kutokana na kazi kubwa wanayofanya ya kuhakikisha jamii inapata elimu kuhusu madhara ya kutoa na kupokea rushwa," alisema.
Aliwataka wanafunzi hao kuongeza bidii katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia klabu za wapinga rushwa zilizoanzishwa katika shule za msingi, sekondari hadi vyuoni nchini.
Ussi, alisema wakifanya hivyo, watasaidia kwa kiasi kikubwa kuielimisha jamii kupinga rushwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde, aliwapongeza wanafunzi wa shule hizo kwa mdahalo huo kulenga rushwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mavunde, alisema uwezo wa wanafunzi hao umeonesha jinsi gani klabu za wapinga rushwa zilizopo katika shule mbalimbali zinasaidia kufahamu madhara ya kutoa na kupokea rushwa katika Uchaguzi Mkuu.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabiry Shekimweri, alisema lengo la kuanzisha klabu hizo shuleni ni kutengeneza mabalozi wazuri kusimama imara kukemea rushwa nchini baada ya kuhitimu masomo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mdahalo Mkoa wa Dodoma, Fransisco Magoha, alisema ni mwaka wa tatu wanaendesha mdahalo huo na kuwa chachu kwa wanafunzi kujiunga na klabu za wapinga rushwa katika shule na vyuo wanavyosoma.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED