Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limetangaza nafasi za kuandikishwa jeshini kwa vijana wenye elimu ya sekondari hadi vyuo vikuu, asilimia 90 zikielekezwa zaidi kwa madaktari bingwa na wabobezi wa binadamu kwa hospitali zake.
Hayo yalibainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda, leo wakati akitangaza nafasi za kuandikisha vijana hao kwa ajili ya kujiunga na jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya JWTZ Msalato nje kidogo ya Jiji la Dodoma, Kanali Ilonda, amesema uandikishaji vijana hao, utahusishwa wa Kitanzania wenye taaluma adimu kwa ajili ya kupewa mafunzo ya kijeshi, ikiwemo kuendeleza taaluma zao.
Amesema watakaopata nafasi kwa upande wa taaluma ya tiba baada ya kuhitimu mafunzo hayo, watapelekwa katika hospitali mpya ya jeshi hilo iliyokabidhiwa hivi karibuni kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda na nyingine ili kusaidia kutoa huduma za afya kwa jamii.
Amezitaja nafasi hizo kuwa ni pamoja na taaluma ya tiba kwa madaktari wabobezi na bingwa wa magonjwa mbalimbali.
Ilonda, ametaja taaluma nyingine kuwa ni ya uhandisi, mafuta, ufundi mchundo na hali ya hewa.
Hata hivyo, amesema kwenye fani ya mafundi waombaji wanatakiwa wawe na vyeti vinavyotambulika kisheria.
Amezitaja sifa za waombaji kuwa awe raia wa Tanzania mwenye Kitambulisho cha cha Taifa (NIDA), akili timamu na afya njema.
Awe na nidhamu, hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai mahakamani, kufungwa, awe na cheti halisi cha kuzaliwa, shule na vya taaluma.
Nyingine awe na hajawahi kutumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) na kuhitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mkataba wa kujitolea au kwa mujibu wa sheria na kutunukiwa cheti.
Kwa vijana wenye elimu ya kidato cha nne na sita, awe na umri usiozidi miaka 24, Stashahada 26 na wenye elimu ya juu 27.
Kwa mujibu wa Ilonda, kwa upande wa madaktari bingwa wa binadamu, umri unaotakiwa usizidi miaka 35.
"Hakumzuii mtu asiye na cheti cha mafunzo ya kujitolea ya JKT kuomba nafasi ya kuandikishwa," amesema.
Amesisitiza kuwa idadi ya watu wanaohitajika italingana na ya watakaokidhi vigezo vinavyohitajika na jeshi hilo kwa waombaji.
Ametoa tahadhari kwa jamii kutorubuniwa kutoa fedha yoyote ili wapate nafasi ya kuandikishwa na kuonya watakaobainika kudanganya umma kuhusu nafasi hizo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED