WAKALA wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) umetengewa zaidi ya shilingi trilioni 1.19 kwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara nchini kwa mwaka wa fedha wa 2025/26.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahim Kibasa, amesema hayo kwenye Maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mahali pa Kazi Duniani, yanayofanyika kitaifa mkoani hapa, kwenye viwanja vya Mandewa mjini, yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA).
Kibasa, amesema fedha hizo zinatarajia kutumika kwa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 893.16 na za changarawe 12,000 nchi nzima.
Amesema bajeti hiyo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na shilingi bilioni 246 ambazo TARURA ilitengewa mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Ameeleza fedha hizo zinatokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo mfuko wa barabara, tozo za mafuta ya petroli na diseli, miradi ya uboreshaji wa miji (TACTIC), Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu Dar es Salaam (DMDP).
"Serikali inaendelea kuhakikisha barabara ambazo zipo katika kila halmashauri zetu zinafunguliwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji maeneo ya wananchi," amesema.
Kibasa, amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, TARURA ilipangiwa kutumia shilingi bilioni 886.3 na kujenga barabara za kilomita 278.32 za lami na kilomita 9334 changarawe.
Kibasa, amesema TARURA imekuwa ikitumia mawe kujenga madaraja kwa kutumia mawe ili kupunguza gharama.
Amesema hadi sasa madaraja 401 yamejengwa nchini, kati ya hayo 34 yako mkoani Singida.
Amesema Kigoma unashika nafasi ya kwanza kwa kujenga madaraja mengi ya mawe ukifuatiwa na Arusha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED