TAASISI isiyo ya kiserikali ya Jamii Kwanza Initiative (JKI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Amani Kata ya Kipunguni, wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam, imetoa mafunzo kwa wanawake wapatao 150 kuhusu kuepukana na athari ya mikopo kandamizi (kausha damu), ili kuwawezesha kuondokana na adha na udhalilishaji wanazozipata.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa (JKl), Daniel Migera, amesema kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo, ili kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi.
Amesema serikali imeweka mipango ya kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi, kwa kuwapatia mikopo ya asilimia 10, hivyo kwa mafunzo wanayoyatoa watapata elimu ya fedha ambayo itawasaidia kwenye biashara zao.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kipunguni, Gamaliel Mhanga, ameishukuru na kuipongeza JKI na Mwenyekiti wa mtaa huo, kwa kutoa mafunzo hayo kwani jambo hilo ni zuri na lipo kwenye ilani ya CCM ambayo inatekelezwa bila ubaguzi kwa wananchi.
Aidha ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kusikiliza kwa makini, kuuliza maswali pale wasipoelewa, ili baadae waweze kuyafanyia kazi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Abdi Mahanyu amesema kuwa lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuwa Fanya wanawake kuwa na maisha bora na kuepukana na mikopo kandamizi (kausha damu).
"Leo tumeanza mafunzo haya kwa takribani wanawake 150, tutawafunza ili kuvunja minyororo ya mikopo isiyo na tija," amesema Mahanya.
Mmoja wa washiriki, Mkuu Ramadhani, amesema mafunzo hayo yamewaonesha mwanga kwani kabla ya kupewa mafunzo yatawawezesha kufanya biashara, bila kutegemea mikopo kandamizi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED