Dk. Kitima: Kukemea wizi wa kura si siasa, ni wajibu wa kidini na kimaadili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:08 PM Apr 29 2025
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Dk. Charles Kitima,
Picha:Mtandao
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Dk. Charles Kitima,

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Dk. Charles Kitima, amesema kuwa jukumu la viongozi wa dini kukemea maovu katika jamii, likiwemo wizi wa kura na ukiukwaji wa misingi ya haki katika chaguzi, si kuingilia siasa bali ni kutimiza wajibu wa kidini na kimaadili waliokabidhiwa na Mwenyezi Mungu.

Akizungumza na DW Swahili hivi karibuni, Dk. Kitima alisema kuwa viongozi wa dini hawana wajibu wa kuwaambia wananchi wachague chama au mgombea fulani, bali wana wajibu wa kueleza ukweli na kukemea vitendo viovu vinavyofanywa na watu au taasisi yoyote ile, hasa vinavyohatarisha haki, amani na ustawi wa taifa.


"Sisi kazi yetu kama Kanisa ni kukemea uovu. Kuiba kura za wananchi, kupeleka kura zisizo halali yaani feki, kumtangaza mtu ambaye hajapata kura nyingi, unamuacha aliyepata nyingi—huo ni uovu," alisema Dk. Kitima


Alibainisha kuwa maovu hayo si suala la kisiasa bali ni suala la kimaadili na kidini, kwani hata katika dini zote zilizopo nchini ikiwemo Ukristo, Uislamu na dini za jadi, kuna misingi ya wazi inayokemea uovu, dhuluma na udanganyifu wa aina yoyote.

"Tanzania ina dini za kimila, Ukristo, Uislamu... katika dini zote hizo Mungu anaagiza maovu ni haya na haya... na hayo ni pamoja na kuiba kura, kuvuruga matokeo, na kutoheshimu sauti ya wananchi. Huo ni uovu wa wazi." alieeleza.


Dk. Kitima alisema kuwa viongozi wa dini hawahitaji ruhusa ya serikali wala vyombo vingine ili kusema ukweli au kukemea dhambi, na kwamba hakuna mamlaka yoyote inayopaswa kuwazuia kuonya au kuelekeza jamii katika maadili na haki.

"Tutakaposema wachague chama hiki au waache chama hiki hapo ndipo tutakuwa tumeingia kwenye siasa. Lakini tunaposema acha kuiba kura, acha kuvuruga kura ya raia- hapo tunatekeleza wajibu wa kidini." alisema.


Dk. Kitima alisisitiza kuwa taifa limekubaliana kupitia sheria na katiba yake kwamba maamuzi ya wananchi yaheshimiwe, na kuwakumbusha walioko madarakani kutekeleza majukumu yao kwa haki bila ubaguzi. 

"Tenda kadiri wananchi mlivyokubaliana kama nchi. Heshimu maamuzi ya wananchi. Kuwambia waheshimu maamuzi ya wananchi siyo kuingilia siasa—ni kuwaambia watende haki."