Dk. Ndumbaro: Mabalozi CCM tumieni mafunzo kisheria kutatua migogoro

By Gideon Mwakanosya , Nipashe
Published at 07:03 PM May 08 2025
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, amewataka mabalozi na wajumbe wa mashina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Manispaa ya Songea kutumia vyema mafunzo ya kisheria na uongozi wanayopatiwa ili kusaidia kutatua migogoro mbalimbali inayojitokeza katika maeneo yao.

Dk. Ndumbaro, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, ametoa kauli hiyo leo Mei 8, wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa mabalozi na wajumbe zaidi ya 500 katika Ukumbi wa Bombambili, Songea. Mafunzo hayo yanaendeshwa na Wizara ya Katiba na Sheria.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuleta mabadiliko ya kweli na endelevu kwa wananchi kwa kuwajengea uwezo wa kuelewa na kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii zao.

Aidha, Dk. Ndumbaro amesema mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kuelewa umuhimu wa kuchagua viongozi bora katika Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, na kutumia fursa hiyo kuwaomba washiriki kumpa kura za kishindo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea mwenza Dk. Emmanuel Nchimbi.

Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakieleza kuwa yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutatua migogoro iliyokuwa ikiwakabili katika maeneo yao.

1