KATIKA dhana kuu, suala la mafanikio ya miradi ya maendeleo katika jamii, hutegemea kwa kiasi kikubwa kiwango cha ushirikishwaji jamii.
Sehemu kubwa ya washiriki wa maendeleo ndani yao vijana, ndani yao kuna kundi kubwa la walio na jinsia ya kike ambao katika nafasi yao kijinsia, wana umuhimu wao.
Vilevile, katika mgawanyo mkubwa wa kijamii, wana nafasi kubwa kutafsiri mustakabali wa jamii katika mjumuiko wa kimaisha.
Ni bahati mbaya kundi hilo la vijana ndilo athari za matumizi ya dawa za kulevya, linakumbwa na changamoto kubwa kama vile athari za matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, walio katika jinsia ya kike wanakabiliwa na athari za ziada, zinazojumuisha mimba na ndoa za utotoni, huku zikikwama kupata suluhisho sahihi.
Hapo katika hatua za awali, mara moja wanakwama kushiriki katika hatua za kimaendeleo kitaifa.
Ni aina ya mustakabali unaokutana na uhalisia mwingine, kwamba katika zama zilizoko sasa ndani ya mabadiliko ya kijamii na kisiasa, ushirikishwaji wananchi unazidi kushika kasi katika maendeleo endelevu.
Ushirikishwaji huo hauishii katika kushiriki uchaguzi au mikutano, bali unahusisha nafasi ya wananchi kutoa maoni, kueleza changamoto zinazowakabili na kushiriki kutafuta suluhisho.
HALI HALISI
Hadi sasa takwimu zinaonyesha namna ukatili wa kijinsia ulivyo katika picha mbaya, Ripoti ya Jeshi al Polisi ya Mwaka 2023, ikidhihirisha kupitia Dawati la Jinsia na Watoto, zaidi ya matukio 29,000 ya ukatili wa kijinsia yaliripotiwa kote nchini yakihusisha vipigo, ubakaji, ulawiti na ukatili wa kiuchumi.
Inapewa ufafanuzi wa kiuchambuzi kwamba, wananchi wengi wamekuwa wakinyamaza kutokana na hofu, kukosa elimu au kutokuamini vyombo vya sheria.
Mtazamo wa maoni, unaelekeza kuwa kuwa uhuru wa kujieleza unapobaki kupitia majukwaa ya wazi kama radio za kijamii, au mikutano ya mtaa, basi hatua sahihi zingechukuliwa kufikia ngazi ya ufanisi zaidi.
MIMBA NA NDOA
Hadi sasa mimba na ndoa za utotoni, ni changamoto inayokwamisha maendeleo ya wasichana nchini na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Idadi ya Watu (UNFPA) zinaonyesha asilimia 36 ya wasichana nchini Tanzania huolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18, huku asilimia 27 wakipata mimba wakiwa katika umri wa shule.
Katika ripoti ya mwaka 2022 iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), maeneo ya mikoa kama Shinyanga, Tabora na Mara yameendelea kuongoza mikasa ya mimba na ndoa za utotoni.
Sababu kubwa inatajwa ni ukosefu wa elimu sahihi kwa wazazi na jamii, pamoja na kuwapo mila kandamizi, kukipewa mapendekezo ya elimu kwa wananchi, hususani wazazi, viongozi wa kimila na vijana, inaweza kusaidia mabadiliko.
Hiyo inaendana na kuanzishwa mijadala ya wazi na kampeni jamii.
Ni muktadha unaogusa pia suala ka matumizi ya dawa za kulevya nchini, jamii zimekuwa zikiathirika kimwili, kiakili na hata kiuchumi, taifa likipoteza nguvu kazi na kuwekeza fedha nyingi katika matibabu kwa waraibu wa dawa hizo.
Kamishna Jenerali Aretas Lyimo, wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA), akinena: “Watu millioni 28 nchini walipatiwa elimu kuhusu athari za dawa za kulevya”
Mafanikio ya miradi ya maendeleo ya kijamii yamekuwa yakitegemea kwa kiasi kikubwa kiwango cha ushirikishwaji jamii, darasa mfano ni programu “Tuwalinde Watoto" inayotekelezwa na shirika Plan International, ikishirikiana na serikali mitaa.
Ni programu inayotajwa kufanikiwa kupunguza vitendo ukatili dhidi ya watoto katika baadhi ya maeneo mkoani Geita, ikishirikisha wazazi, walimu, viongozi wa dini na watoto wenyewe wanaishuhudia kinachoendelea.
Ni dhihirisho inalotajwa kuwa jamii inapopewa nafasi ya kusema inachangia kupatikana suluhuhishi ya kimandeleo dhidi ya vikwazo mbele yao, hali inayoacha dhirisho kuwa serikali na wadau wa maendeleo hawapaswi kuchukua nafasi ya wananchi, bali kuwawezesha, kuwahamasisha na kuwaunga mkono watende.
Katika muktadha huo, inatajwa kuwa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), unahitaji msisitizo wa ushiriki wa jamii nzima.
DARASA LA NGO
Ni katika sintofahamu ya namna hiyo, kuna mfano wa shirika binafsi liitwaalo Medea Tanzania limejipambanua kuleta mwelekeo mpya kitafiti, ushirikishwaji jamii na kuunda majawabu yenye uhalisia wa matatizo ya wananchi, kupitia mradi “Jenga Sauti”.
Kwa kutumia mbinu bunifu za usanii, vyombo vya habari na simulizi zenye ukweli wa maisha ya watu, Medea inachora ramani mpya ya maendeleo kufikia suluhisho la moja kwa moja kwenye vinywa vya wahanga na mashuhuda wa changamoto za kijamii.
Mkoani Arusha, eneo ni linaloelezwa kuwapo ongezeko la matatizo sugu matumizi ya dawa za kulevya, ndoa na mimba za utotoni, pia ukeketaji wasichana.
Sasa, asasi hiyo imeanza kukutana na baadhi ya mashirika yanayotekeleza majukumu yake mkoani humo, kusaka ili kuzungumza lugha moja ya suluhu.
Edna Kalula, Ofisa Mradi wa Medea, anafafanua wamejipanga na mradi unaolenga utoaji elimu kupitia vipindi simulizi kwenye vyombo vya habari vya kanda Kaskazini; Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
“Katika wilaya ya Arumeru na Arusha Jiji mkoani Arusha, ni miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kunufaika moja kwa moja na mradi huu, jamii itapata fursa ya kujifunza kupitia hadithi halisi za wahusika walioguswa na madhara ya changamoto hizi,” anasema Edna.
Kwa mujibu wa Edna, lengo la mradi haishii utoaji elimu kwa mtazamo wa kitaalamu tu, pia kushirikisha jamii kutoa majawabu yao.
“Tunapokwenda kuzungumza na wananchi wa maeneo haya, tunasikiliza simulizi zao, tunagusa maisha yao, kisha tunaleta hadithi hizo kwenye majukwaa ya redio, mitandao ya kijamii na mikutano ya wazi ili kila mtu apate kujifunza na kuchukua hatua,” anasema Edna.
Ni mtazamo shirikishi ambao Medea inaamua kuoga hatua ya ziada, kuvika wadau wengine walikofika.
“Medea imeamua kwenda mtaani, porini na vijijini pale ambapo matatizo yanatokea, na kuyasikia kutoka kwa wahusika,” anasema Edna, akiitaja “ni kazi inayohitaji ujasiri, lakini pia huruma kwa wananchi.”
CHANGAMOTO & UTATUZI
Anataja eneo mojawapo la changamoto tajwa, ni mila ya kijamii ikiweka kikwazo, hali kadhalika namna ya kuvunja mila hiyo ya karne nyingi, kwa dhana “matendo kama ukeketaji na ndoa za utotoni kutokuwa jambo la kuzungumzia hadharani katika jamii wahusika.”
Mbinu mpya inayotumiwa na Medea sasa kuvunja mpaka huo wa kimila na ukimya wake ni kubeba makusanyo ya kauli na dodosa zake, kisha kuanikia umma, hata inaamsha mjadala wenye kuchochea mabadiliko ya kweli.
Anavitaja vipindi vinavyoundwa redioni vinakusudia kufikia walengwa kupitia lugha na mazingira yao, akitumia mifano ilivyoonyesha mafanikio chanya katika maeneo mengine ya nchi, kama vile mikoa ya Kigoma, Tabora na Lindi ambako hilo wamelianikisha.
Anasema katika jamii yoyote ile, kutambua mizizi ya tatizo ni hatua ya kwanza kuelekea tiba. Kama jamii inakabiliwa na matumizi ya dawa za kulevya, ni lazima kuelewa kwa nini vijana wanajitumbukiza kwenye mtego huo.
Edna anahimza umuhimu wa jamii kuulizwa jamii mzizi wa matatizo yao na majibu ya kuyatatua, akigusa mfano wa maeneo kama ndoa za utotoni, matumizi ya dawa za kulevya na hata ukeketaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED