Dk. Simba: Ilani ya CCM imejali maslahi ya wananchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:09 PM Jun 03 2025
Dk. Simba: Ilani ya CCM imejali maslahi ya wananchi
Picha:Mtandao
Dk. Simba: Ilani ya CCM imejali maslahi ya wananchi

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka Mkoa wa Morogoro Mjini, Dk. Ally Simba amekipongeza chama hicho kwa kutoka Ilani bora ya uchaguzi inayojali maslahi ya wananchi na taifa.

Hivyo, amewataka wanachama wa CCM kuisoma kwa undani na kuielewa kikamilifu pamoja na kuitangaza, hususani wakati huu ambapo taifa linapokaribia kufanya Uchaguzi Mkuu.

Akizungumza na Nipashe Digital, Dk. Simba ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano la Afrika Mashariki amesema ilani hiyo imebeba matumaini makubwa.

Dk. Simba amesema ilani hiyo inatambua kuwa maendeleo lazima yaanzie ngazi ya chini ikionesha kuwa ni kwa namna gani inaheshimu ukweli kwamba "siasa ni ya wananchi wa kawaida", na watu lazima wajione ndani ya ahadi zinazotolewa. 

Amesema kimsingi nguzo kuu za ilani mpya inajengwa kwa misingi ya mageuzi ya kisasa ya uchumi jumuishi, shindani na unaotegemea kuongeza thamani ya rasilimali za ndani, huku ikiongeza fursa za ajira kwa vijana, kipato na kupunguza umaskini.

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka Mkoa wa Morogoro Mjini, Dk. Ally Simba.

"Hii ni dira yetu ya kisiasa. Tunapaswa kuilinda kwa hoja, shauku, unyenyekevu wakati wa kampeni. Tuanze kujipanga kwa utekelezaji wake, wana CCM tuna kila sababu ya kuamini kuwa kwa ilani hii, mgombea wetu wa nafasi ya urais, Dk. Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza, Dk. Emmanuel Nchimbi wataibuka na ushindi wa kishindo," amesema Dk. Simba.

Amesema ilani pia imezingatia kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii kwa kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, sambamba na kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia.

Amesema ilani hiyo inazungumza lugha ya kawaida, inagusa mahitaji ya kila mwananchi na kuakisi falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya “Kazi na Utu”. Hivyo aliwataka kila mtu kufanya kazi kwa kuheshimu na kuthamini utu wa kila mmoja. 

Dk. Simba amesema ujasiri, uwazi na hekima ya kitaifa ya Dk. Samia Suluhu Hassan inamfanya kuwa zaidi ya muhamasishaji na mbadilishaji wa mustakabali wa taifa.

Aidha, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwahamasisha Watanzania kutokana na uongozi wake imara, huku akiahidi kumsaidia katika safari ya kuwapatia watanzania heshima, fursa na mshikamano.