Jafo ahimiza wananchi kujali miundombinu ya maji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:40 PM Mar 06 2025
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ( Mbunge) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa taasisi ya LALJI FOUNDATION na viongozi wa kata ya Msanga mara baada ya uzinduzi wa mradi wa kisima cha maji
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ( Mbunge) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa taasisi ya LALJI FOUNDATION na viongozi wa kata ya Msanga mara baada ya uzinduzi wa mradi wa kisima cha maji

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, amewataka wananchi wa Kata ya Msanga Wilayani Kisarawe, kushirikiana na serikali kutunza miundombinu ya maji, ili kusaidia jamii na kuleta manufaa kwa taifa.

Kiongozi huyo alitoa wito huo hivi karibuni katika Kijiji cha Mianzi Kata ya Msanga, wilayani Kisarawe mkoani Pwani, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kisima cha maji uliofadhiliwa na taasisi ya Lalji Foundation na Makbur Jaffer Family ambao utawafaidisha wananchi zaidi ya 1,000 wa eneo hilo.

Aidha Waziri Jafo ambaye ni Mbunge wa Kisarawe, ameipongeza Taasisi ya Lalji Foundation, kwa kutekeleza mradi huo wa kisima unaogusa wananchi moja kwa moja, kwa kupata huduma ya maji safi na usalama.

Vilevile, aliwapongeza wananchi wa Msanga kwa kupokea mradi huo, huku akiwataka kutunza miundombinu ya mradi huo, ili uendelee kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Alisema walichokifanya Taasisi ya Lalji, wameitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuwahimiza wadau wa maendeleo kwa kushirikiana na serikali kuisaidia jamii katika mambo mbalimbali, ikiwamo kutekeleza miradi ya maendeleo.

Aidha, aliwataka wadau wengine wa maendeleo kuendelea kuisaidia Kisarawe kwa kuwa bado wananchi wanahitaji huduma mbalimbali za kijamii, hivyo ni vyema wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali kusaidia jamii. 

Mwenyekiti wa taasisi ya Lalji Foundation, Imtiaz Lalji alisema lengo ni kuendelea kufikia jamii zenye mahitaji maalumu, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuitunza miradi hiyo, ili iweze kudumu kwa muda mrefu

Mkazi wa Msanga, Latifa Kondo, alisema mradi huo utapunguza changamoto ya kufuata maji umbali mrefu, ili muda huo wautumie kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na uchumi.

Diwani wa Kata ya Msanga, Zuberi Kizwezwe, alisema msaada huo wa kisima cha maji safi na salama, umekuwa mkombozi kwa wananchi na utawasaidia kutotembea umbali mrefu hadi nyakati za usiku kufuata huduma ya maji.