‘Jamii ijali afya, kuepuka magonjwa’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:37 PM Mar 06 2025
‘Jamii ijali afya, kuepuka magonjwa’
Picha: Mtandao
‘Jamii ijali afya, kuepuka magonjwa’

JAMII imeaswa kuwa na utaratibu wa kutazama afya zao, ili kusaidia kuimarisha uimara wa mwili na kuepukana na magonjwa yasiyo ya lazima pamoja na vifo.

Hayo yalielezwa na Mjumbe wa Bodi kutoka Hospitali ya Mtakatifu Clare, iliyopo Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, Pius Kamala, ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Alisema kwa sasa jamii kubwa hususan waishio maeneo ya Kanda ya Ziwa, wamekuwa wakifika katika vituo vya kutolea huduma za afya mara baada ya kuona magonjwa yamekuwa sugu na kutibika kwake yanahitaji hadi kufika vituo vya huduma za afya.

Katika hatua nyingine alisema kuwa jamii kubwa ya Kitanzaia, imefanya afya kutokuwa sehemu ya utamaduni wao, jambo linalosababisha upotevu mkubwa wa nguvu kazi ya taifa.

Aliwataka akinamama na jamii nzima kuwa na utamaduni wa kuzijali afya zao, kwa kwa kwenda mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma, pia kufanya mazoezi na kula vyakula vya asili na vile vinavyojenga mwili kuwa imara wakati wote. 

Mkurugenzi wa Cheza Kidansi Entertainment, Benard James, alisema wamelenga kuwapongeza wanawake wote nchini kwa kuhenzi utamaduni wa Kitanzaia jambo linalopelekea taifa kupata wageni wengi kupitia shughuli za utalii na kuingiza mapato.

Alisema pia jamii haiwezi kuzungumza suala la utamaduni, bila kuzungumzia utalii maana taifa limekuwa likikuza pato kupitia utalii wa ndani na wa nje.

Aziza Steven ni mkazi wa mtaa wa Mlango Mmoja, jijini Mwanza, alisema kuwa wanawake wanapaswa kupewa haki kama wanaume na baadhi ya wanawake wamekuwa wakikosa haki zao za msingi, huku sababu kubwa ikiwa ni kutokana na utamaduni wa jamii kutothamini mchango wa wanawake nchini.