Kata ya Chuno, wanawake wabeba zege

By Baraka Jamali , Nipashe
Published at 02:36 PM Mar 06 2025
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Shadida Ndile (wa katikati ), akishirikiana na wakazi wa Kata ya Chuno, kumwaga zege katika ujenzi wa msingi wa uzio.
Picha: Baraka Jamali
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Shadida Ndile (wa katikati ), akishirikiana na wakazi wa Kata ya Chuno, kumwaga zege katika ujenzi wa msingi wa uzio.

KUELEKEA maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wanawake wa Kata ya Chuno, wilayani Mtwara wameungana na wananchi wengine katika kumwaga zege, kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa Shule ya Sekondari ya Kata hiyo.

Tukio hilo liliongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Shadida Ndile.

Ndile alitumia fursa hiyo kuwapongeza wanawake wa Kata ya Chuno, kwa kujitoa na kuonesha moyo wa uzalendo kwa kushiriki katika kazi hiyo ya ujenzi. 

Alisema kuwa hatua hiyo ni mfano wa kuigwa na jamii nzima kwani itasaidia kuhakikisha usalama wa wanafunzi na mali za shule hiyo.“Wanawake wa Chuno mmeonesha mfano mzuri sana wa uzalendo na kujitolea. Kumwaga zege na kujenga uzio huu kutaleta faida kubwa kwa wanafunzi wetu kwa kuimarisha usalama wao pamoja na mali za shule,” alisema Ndile.

Mbali na pongezi, Ndile aliahidi kuchangia tofali 1,000 na mifuko ya saruji 100, ili kuongeza kasi ya ujenzi huo. 

Alisema msaada huo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuhakikisha mazingira ya shule yanaboreshwa, ili wanafunzi wapate elimu katika mazingira salama.

Wananchi waliojitokeza walionesha furaha yao na kueleza umuhimu wa kukamilisha uzio huo kwa haraka. Walisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitoroka masomo kutokana na ukosefu wa uzio imara, hivyo kujenga uzio huo kutadhibiti hali hiyo.

Baadhi ya wanafunzi nao walikiri kuwapo kwa changamoto ya utoro na kupongeza juhudi za wazazi wao na jamii nzima katika ujenzi huo. 

Walisema kuwa wanajihisi salama zaidi na wataweza kujikita zaidi katika masomo yao bila wasiwasi.

Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani yanafanyika Machi 8, kila mwaka,  wanawake kote duniani hutambua na kusherehekea mchango wao katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.