Katibu Mwenezi Taifa NCCR Mageuzi ahamia ACT Wazalendo

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 04:17 PM Jun 09 2025
Katibu Mwenezi Taifa wa Chama cha NCCR Mageuzi Elisante Ngoma amekihama Chama hicho na kujiunga na ACT Wazalendo. Elisante amepokelewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu leo Juni 09, 2025.

Aliyekuwa Katibu Mwenezi Taifa wa NCCR Mageuzi, Elisante Ngoma, ametangaza kujiondoa katika chama hicho na kujiunga na ACT Wazalendo, akieleza kuwa NCCR Mageuzi imepoteza dira ya kisiasa na kushindwa kupambana ipasavyo na utawala wa CCM.

Katika tamko lake kwa vyombo vya habari, Ngoma amesema hatua yake imechochewa na kuvutiwa na misimamo ya ACT Wazalendo inayoweka mbele utu, uwajibikaji na maendeleo ya wananchi, pamoja na juhudi za chama hicho kulea viongozi vijana.

“ACT Wazalendo ni chama kinachotoa nafasi kwa vijana, kina dira ya wazi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, na kina dhamira ya dhati ya kuiondoa CCM madarakani,” alisema Ngoma.

Ngoma amesema atatumia uzoefu wake kusaidia harakati za chama hicho hasa katika jimbo la Same Magharibi na maeneo mengine nchini. Alisema sasa ni wakati wa kuandika historia mpya ya kuondoa mfumo wa uongozi wa kiburi, usiosikiliza wananchi.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema kuwa chama cha ACT-Wazalendo kipo kwa ajili ya kupanua wigo na fursa za siasa kwa ajili ya vijana wenye uchu na maendeleo ya nchi yao.