Makalla atoa msimamo wake hatagombea ubunge Mvomero

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 10:54 AM May 08 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, amesema hana mpango wa kugombea ubunge jimbo la Mvomero, na asihesabiwe kwa sasa katika kinyang'anyiro hicho.

Ametoa kauli hiyo baada ya mbunge wa Mvomero (CCM), Jonas Van Zeeland,  kutangaza kwamba endapo Makalla, atachukua fomu kugombea ubunge jimboni humo, 2025, yeye hatachukua, atamuunga mkono.

Ametangaza hilo Mei 7, 2025, katika mkutano wa hadhara unaofanyika wilayani Mvomero, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya siku saba ya Mwenezi mkoani humo.

Akimjibu katika mkutano huo, Makalla akiwa amepiga magoti, amesema anaomba heshima aliyopewa na CCM aifanye kwa asilimia 100.

“Ninawashukuru, 2010 mlinipa nafasi kuwa mbunge wa Mvomero,  2020 mlinipa nafasi kuongoza kura za maoni, yote hii tulifanya kazi vizuri, yapo mambo alifanya mtangulizi wangu Murad Sadiq nikayaendeleza hakuna mtu alijua tutaleta umeme, kujenga barabara na maji.

“Niwaombe kwa heshima kubwa na kwa imani kubwa naomba mniruhusu nafasi aliyonipa Mheshimiwa Rais niwe Msemaji wa Chama nimsaidie Rais ili tuvuke katika uchaguzi mwaka huu.Ninawapenda sana na chama ninakipenda,” amesema na kuwaita jukwaani Sadiq na mbunge wa jimbo hilo.

Amesema  Katibu Mwenezi ndiye anayenadi wagombea na kukisemea chama, na kueleza kuwa akienda Mvomero chama chake kitakuwa kimepwaya.

Awali, Mbunge Zealand amesema katika uchaguzi wa mwaka 2020, Makalla alikuwa wa kwanza, Murad Sadiq, alikuwa wa pili na yeye wa tatu,  na akawa Mbunge Mvomero hadi sasa.

“Kama kuna mtu amenifundisha siasa ya uvumilivu ni Makalla, hakuwa na kinyongo chochote, ninatamka leo, Mungu akiniweka  hai hadi wakati wa kuchukua fomu, kama Makalla utachukua fomu sitachukua fomu.

“Kaka yangu ninakuhakikishia kama utakuja hilo ni lako mwenyewe, haki ya Mungu nitakupa heshima kama ulivyonipa 2020, ni watu wachache wenye moyo wa aina yako,” amesema.

Kadhalika, amemweleza kwamba wanaona namna anavyopiga kazi, anawapiga spana mpaka wanapagawa wanatafutana.