Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amewakumbuka walimu waliomfundisha darasa la kwanza kwa kuwakatia bima kubwa ya afya yenye thamani ya Shilingi milioni 3.2 kwa kila mmoja.
Mavunde alitoa zawadi hiyo kwa Mwalimu Lyndu Muhembano na Mwalimu Dina Mwaluko, waliomfundisha miaka 35 iliyopita, kama ishara ya shukrani kwa mchango wao katika maisha yake.
Akizungumza katika hafla ya kugawa vifaa vya masomo, ikiwemo madaftari 10,000 kwa watoto yatima na wanaoishi mazingira magumu katika shule zote za msingi ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mavunde alisema:
"Nimebahatika kukutana na walimu wangu wa darasa la kwanza na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika maisha yangu. Bila wao, nisingefika hapa nilipo leo. Mwenyezi Mungu awajalie afya njema na baraka tele."
Aidha, aliahidi kuendelea kushirikiana nao kuhakikisha wanaishi vizuri.
"Nimeguswa kuwakatia bima kubwa ya afya ili kuhakikisha wanapata matibabu bila usumbufu wowote, hasa kwa kuwa baadhi yao wamestaafu utumishi wa umma," alisisitiza Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma.
Mbali na kuwashukuru walimu wake, Mavunde aliendelea kuunga mkono sekta ya elimu kwa kugawa vifaa vya masomo kwa wanafunzi wenye uhitaji katika shule za msingi za Dodoma.
Juhudi hizi zimepongezwa na walimu, wanafunzi, na wazazi wa Jiji la Dodoma, wakimuelezea Mavunde kama kiongozi mwenye moyo wa shukrani na anayejali maendeleo ya jamii yake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED