Bodaboda adaiwa kuuawa kwa kufumwa na mke wa mtu

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:36 PM Mar 28 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa.

Mwendesha pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ Mhochi Joseph (29) Mkazi wa Kitangiri wilayani Ilemela mkoani Mwanza anadaiwa kushambiliwa hadi kufariki dunia baada ya kufumaniwa akiwa na mke wa Athumani Morandi(36).

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea Machi 21 katika mtaa wa Gaana wilayani humo.

Kamanda Mutafungwa amesema bodaboda huyo aliuawa kwa kushambuliwa maeneo mbalimbali ya mwili wake baada ya kukutwa amelala na mke wa Morandi ambaye ni dereva.

“Jeshi la polisi lilifanya upelelezi na kufanikiwa kumkamata Athumani Morandi Mkazi wa Gana ambaye anadaiwa kumfumania Mhochi bodaboda akiwa amelala na mke wake kisha kumshambulia kwa kutumia kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za za mwili wake chanzo cha tukio ni wivu wa mapenzi,”amesema DCP Mutafungwa.

Katika hatua nyingine DCP Mutafungwa amaesema jeshi hilo linamshikilia Doto Marco (18) Mkazi waButonga wilayani Sengerema kwa tuhuma za mauaji ya Eliyas John (18).

Kamanda Mutafungwa amesema Marco anadaiwa kumuua John kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali sehemu ya kifuani katika tukio lililotokea Machi 23 majira ya saa nne usiku katika mtaa na kisiwa cha Kome.

“Yalizuka mabishano baina yao na kisha ugomvi ambako Marco inadaiwa kuwa alishikwa na hasira na kumchoma mwenzake Mtuhumiwa tayari amehojiwa na upelelezi utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,”amesema DCP Mutafungwa.