TARURA kurejesha mawasiliano barabara ya Vibao Vitatu Babati

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 05:13 PM Mar 28 2025
TARURA kurejesha mawasiliano barabara ya Vibao Vitatu  Babati
Picha: Mpigapicha Wetu
TARURA kurejesha mawasiliano barabara ya Vibao Vitatu Babati

Baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani Babati, Manyara, kusababisha uharibifu wa pande mbili za Daraja la Mto Kiongozi katika barabara ya Vibao Vitatu, Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) wamewahakikishia wananchi kuwa mawasiliano ya barabara hiyo yatarejeshwa haraka.

Akizungumza na Nipashe Digital kwa njia ya simu, Kaimu Meneja wa TARURA, Mhandisi Naftali Lyatuu, amethibitisha kuwa kilichotokea ni udongo kuporomoka na siyo daraja lenyewe kubomoka.

"Ni udongo tu ulioporomoka, siyo daraja lililobomoka. Mvua zikikata, ndani ya wiki moja tutarejesha mawasiliano hayo. Wananchi wasiwe na wasiwasi," alisema Mhandisi Lyatuu.

Naye Mbunge wa zamani wa Babati Vijijini, Vrajil Jituson, akizungumza na Nipashe Digital kwa njia ya simu, alisema kuwa daraja lililoingiliwa na maji liko mita 700 kutoka barabara kuu ya Babati - Arusha.

Jituson alieleza kuwa upande mmoja wa daraja umetoka kabisa, huku upande wa pili ukiwa umeharibika nusu, hivyo kwa hali ilivyo, barabara hiyo haiwezi kutumika hadi ifanyiwe matengenezo.

"Mtu akitoka Kata ya Kiru hadi daraja hilo ni kilomita 14, hivyo wale wasiokuwa na taarifa wanaweza kufika eneo hilo na kushindwa kuvuka," alisema Jituson.

TARURA imewataka wananchi kuwa na subira wakati juhudi za kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo zikiendelea.