Vijiji Handeni kujengewa mradi wa maji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:24 PM Mar 28 2025
Vijiji Handeni kujengewa mradi wa maji
Picha: Mtandao
Vijiji Handeni kujengewa mradi wa maji

SHIRIKA la World Vision Tanzania linatarajia kujenga mradi wa majisafi na salama katika vijiji vilivyopo wilayani Handeni Mkoa wa Tanga na kunufaisha watu 3,890 .

 Mkurugenzi wa Operesheni wa shirika hilo, Nesserian Mollel, alisema mradi huo unatarajiwa kugharimu Shilingi milioni 50 kuunga mkono jitihada za serikali za kuendelea kuboresha sekta ya maji nchini.

Mollel, alisema mradi huo unalenga kutoa maji safi na salama kwa wakazi hao, wakiwemo watoto 2,139. 

Alisisitiza fedha hizo zitatumika kuchimba kisima, kufunga mfumo wa pampu za maji unaotumia nishati ya jua, kujenga tangi la kuhifadhi maji, kuanzisha mtandao wa maji na kusambaza katika Kijiji cha Kwedizinga.

 "Kupitia mradi huu tutahakikisha Kijiji cha Kwedizinga nao watanufaika na mradi huo, dhamira yetu ni kufikia jamii nyingi zenye uhitaji ili kujaza mapengo katika juhudi za wadau wengine kwenye utoaji huduma za maji safi na salama," alisema.

 Kwa mujibu wa Mollel, shirika hilo kupitia wadau wake nchini kwenye sekta ya maji kwa kushirikiana na serikali, limetoa huduma ya maji watu takribani milioni 1.2 nchini

 Shirika hilo pia lilizindua mifumo mipya ya maji katika Kijiji cha Mwatumbe kilichopo Shishiyu Wilaya ya Maswa mkoani Shinyanga na Mahaha kilichopo Endabash, Wilaya ya Karatu (Arusha) na kushiriki katika shughuli za kitaifa.