Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, leo amezindua rasmi Bodi mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kutoa maelekezo mahsusi kuhusu usimamizi wa Mfuko huo kwa ufanisi na uwajibikaji.
Katika hafla hiyo, Kikwete amesisitiza umuhimu wa Bodi hiyo kuhakikisha uwekezaji wa Mfuko unaleta tija, kuimarisha usimamizi wa mipango yake, na kuzingatia maadili katika utendaji wake.
"Bodi hii inapaswa kuhakikisha PSSSF inafuata sera, sheria, na kanuni zilizowekwa, pamoja na kuzingatia miongozo ya serikali. Uwajibikaji, uadilifu, ubunifu na ushirikiano ni nguzo muhimu kwa mafanikio ya Mfuko huu," amesema Waziri Kikwete.
Aidha, amehimiza Bodi kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha hakuna mianya ya rushwa miongoni mwa watumishi na viongozi ili kudumisha uendelevu wa Mfuko na kuimarisha uhimilivu wake kwa manufaa ya wanachama wake.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo,Joyce Mapunjo, ameshukuru kwa uteuzi wa wajumbe wa Bodi, akisema kuwa umelenga kuleta uwiano wa kitaaluma unaohitajika kwa maendeleo ya Mfuko.
"Uteuzi wa wajumbe umezingatia taaluma zote muhimu, na tuko tayari kufanya kazi kwa bidii. Tunaahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na tumejipanga kuhakikisha tunafanya kazi kwa kasi kubwa ili kuleta matokeo chanya," amesema Mapunjo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru, ameeleza kuwa Mfuko uko katika mwelekeo mzuri na una rasilimali za kutosha kuhakikisha unatoa huduma bora kwa wanachama wake.
Uzinduzi wa Bodi hiyo mpya unaleta matumaini mapya kwa wanachama wa PSSSF, huku ikitarajiwa kuimarisha ufanisi wa Mfuko huo katika kusimamia mafao ya wastaafu na kuhakikisha ustawi wa sekta ya hifadhi ya jamii nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED