Kongamano kubwa la wanavyuo kutoka vyuo mbalimbali mkoani Dodoma, lililoandaliwa na Kampeni ya Mama Asemewe chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Kiliba, litafanyika tarehe 29 Machi 2025 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre.
Lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wasomi kwa ajili ya kujadili na kuweka maazimio ya pamoja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Hii ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia kwa msingi wa uelewa na uzalendo kwa taifa.
Mwenyekiti wa kampeni hiyo, Geofrey Kiliba, ataongoza mchakato wa maazimio hayo, ambapo wanavyuo watatoa mtazamo wao kuhusu mustakabali wa Tanzania na namna vijana wanavyoweza kushiriki katika kujenga taifa imara kupitia uchaguzi huu muhimu.
Akizungumza kuhusu kongamano hilo, Kiliba alisema:
"Wasomi wana nafasi kubwa katika kuleta maendeleo ya taifa letu. Hili si tu kongamano la mijadala, bali ni jukwaa la kuweka maazimio yatakayoonyesha msimamo wa wanavyuo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Tunataka vijana waonyeshe uzalendo, wawe sehemu ya maamuzi, na wahakikishe kwamba maendeleo yanakuwa ajenda kuu katika uchaguzi wa 2025."
Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa vyuo vikuu, wanazuoni, pamoja na wadau wa maendeleo na demokrasia nchini.
Tukio hilo limepewa kipaumbele maalum kama sehemu ya harakati za kuhakikisha sauti ya vijana wasomi inasikika katika ujenzi wa taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED