KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Peter Msigwa, amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamekuja na mkakati butu, ulioshindikana kabla ya kuanza na dhaifu wa kukimbia uchaguzi wakisema No Reform No Election.
Mchungaji Msigwa amesema hayo jijini Mbeya katika ziara ya siku tatu ya Katibu wa Itikadi na Uenezi na Mafunzo Taifa, CPA Amos Makala, ikihusisha mikoa ya Mbeya na Iringa.
Katika mkutano wa hadhara unaoendelea uwanja wa Ruanda Nzovwe, jijini hapa, Mchungaji Msigwa amewataka wananchi wasikubaki kuingia kupinga uchaguzi.
“Hawana uwezo huo, hawana rasilimali watu, rasilimali fedha na wao wenyewe wamegawanyika.“Mwenyekiti wao alisema anataka kufanya mabadiliko, moja ni ukomo wa uongozi bado hajafanya, ukomo wa viti maalum hawajafanya, wametoka kwenye uchaguzi wamegawanyika,” anasema.
Msigwa anasema wakati anakihama CHADEMA alisema ndani ya chama kuna ufisadi na hakuna demokrasia na hadi sasa mambo hayo bado yapo.
Amesema ili wawe na uhalali wa kusimama kuitaka serikali kufanya mabadiliko, wanatakiwa waanze kwenye chama chao badala ya kuanzisha mapambano ya kuporosha Watanzania.
“Hawana sifa ya kutufundisha.Maendeleo ni mchakato na mabadiliko ni mchakato, kukomesha biashara ya utumwa ilichukua muda mrefu, hata miaka ya 50 na 60 wanawake walikuwa hawaruhusiwi kupiga kura wamedhalilishwa kwa karne nyingi.
“Kubadilisha mtazamo huo imechukua muda..hata mabadiliko katika nchi hii si kweli CCM haijakubali mabadilko, yako na yamefanyika makubwa.“CHADEMA hakina hati miliki ya kweli ya namna ya kuiendesha Tanzania, hati hiyo inamilikiwa na Watanzania wote.Madai wanayoleta wanaona yako sawa lakini hayawezi kuwa sawa kwa kila mtu.
Msigwa amesema wanataka mabadiliko ya kutaka madaraka.
“Huwezi kusikia wanazungumzia matatizo ya wananchi kwenye kilimo, afya, maboresho ya anga..hutawasikia wakizungumzia maboresho ya usafiri wa treni, watazungumzia namna ya kuingia madarakani.
Amesema CHADEMA na vyama vingine vinajulikana kwa kupinga lakini CCM kinajulikana kwa kazi inachofanya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED