Mawakili wa Lissu wahoji amri ya kuzuiwa kwa umma mahakamani

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 05:12 PM Apr 24 2025
 Kiongozi wa Chama cha  People Liberation Party (PLP), cha nchini Kenya Martha Karua (katikati) akizungumza na mawakili wa utetezi wa hapa nchini.
Picha: Grace Gurisha
Kiongozi wa Chama cha People Liberation Party (PLP), cha nchini Kenya Martha Karua (katikati) akizungumza na mawakili wa utetezi wa hapa nchini.

Jopo la mawakili zaidi ya 20 linalomtetea Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini, limetaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa majibu kuhusu ni nani aliyetangaza amri ya kuzuia watu, wakiwemo waandishi wa habari, kuingia kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Mpare Mpoki, akizungumza kwa niaba ya jopo hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, amesema kitendo cha polisi kuzuia watu kuingia mahakamani ni kuingilia uhuru wa Mahakama, na kimekiuka misingi ya haki kwa kutumia nguvu kupita kiasi—hali iliyopelekea baadhi ya watu kujeruhiwa na wengine kukamatwa.

"Tunataka majibu matatu: Ni nani alitoa amri hiyo? Kwa nini ilitolewa? Na ni nani aliyesimamia utekelezaji wake? Bila majibu haya, Mahakama itakuwa inapoteza imani kwa wananchi," amesema Mpoki.

Kwa upande wake, Wakili Alute Mghwai ambaye pia ni ndugu wa Lissu, alieleza kuwa hali anayoishi Lissu akiwa gerezani ni kama tayari ameshahukumiwa, jambo linalokiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. "Haiwezekani Mteja wangu ahamishwe kutoka Gereza la Keko kwenda Ukonga bila taarifa yoyote. Hata sisi hatukupewa taarifa kuhusu alipo," amesema kwa uchungu.

Naye Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Rugemeleza Nshala, ameeleza kuwa hali hiyo ni ya kusikitisha na aibu, kwani hata wao waliweza kuingia mahakamani kwa sababu tu ni mawakili. Alisema wananchi wa kawaida hawakuruhusiwa kuingia, jambo linalozua maswali kuhusu uwazi wa mchakato wa haki.

Kwa mujibu wa mashtaka, Lissu anadaiwa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, alitoa matamshi ya uchochezi kupitia mtandao wa YouTube kwa lengo la kuwashawishi wananchi kuzuia uchaguzi mkuu wa Tanzania. Katika video hiyo, Lissu alinukuliwa akisema:

"Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi... huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana."