‘Mfungo Ramadhani usitumike kisiasa’

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 02:52 PM Mar 06 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha
Picha: Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amewaonya wanasiasa kwamba katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wasitumie mwanya huo kujinufaisha kisiasa, kwa kigezo cha kuandaa futari, kwa ajili ya kufuturisha.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi MachaMwezi huu waumini ya dini ya kiislamu wapo kwenye mfungo wa Ramadhani, pamoja na wakristo kufunga Kwaresma.

Amebainisha hayo, wakati akizungumza na vyombo vya habari, kuwa waumini kufunga ni kuwa karibu na mungu wao kwa ajili ya kufanya toba, hivyo si vyema funga hizo zikaanza kutumika kisiasa, kwa wanasiasa kuanza kuandaa futari na kupenyeza mambo yao ya uchaguzi.

“Mwaka huu kuna uchaguzi mkuu, hivyo wanasiasa wasitumie fursa hii ya mfungo kwa kufuturisha, ili kukidhi haja zao za kisiasa kwa kutenda mambo yenye viashiria vya rushwa,” amesema Macha.

Aidha amewaomba waumini wa dini ya kiislamu na kikristo, kutumia kipindi hiki cha mfungo, kuombea taifa amani hasa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, pamoja na kutumia sadaka zao kuwakumbuka watu wenye uhitaji.

Katika hatua nyingine amewataka wafanyabiashara, waache kupandisha bei ya bidhaa sokoni, ili wananchi wamudu kununua chakula na kufanya funga yao iwe yenye tija.

Caption: