Mgombea nafasi ya Urais kupitia tiketi ya Chama cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele, amesema endapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) itampa ridhaa ya kugombea nafasi hiyo, moja ya vipaumbele vyake ni kuwaandalia wastaafu mazingira bora ya maisha.
Mwaijojele, ambaye aliwasili katika ofisi za INEC majira ya saa 2:59 asubuhi, amesema CCK imeamua kuja na sera hiyo ili kuwaondoa hofu wastaafu, ambapo muda wao unapofika waweze kustaafu kwa amani na kuwaachia nafasi vijana waajiriwe.
Amesema endapo ataingia madarakani, serikali ya CCK itawaondolea kodi watumishi na kuwajengea nyumba ili wanapostaafu wakute makazi yao tayari yamekamilika katika maeneo mbalimbali.
“Watumishi wengi wanaogopa kustaafu kutokana na kuhofia wapi wanakwenda kuishi, wengi wao hawana nyumba, ndiyo maana wanaogopa kustaafu,” amesema Mwaijojele.
Ameeleza kuwa CCK itatekeleza sera ya kukata tozo maalum kwa watumishi, ambazo zitatumika kuwajengea nyumba, ili pindi muda wa kustaafu unapofika waondoke kazini na kupisha vijana waajiriwe.
Mbali na hilo, amesema chama hicho kitaweka mkakati wa kuchangia ujenzi wa nyumba kwa wananchi wa kawaida, ambapo kila mmoja atakatwa kiasi cha fedha mwishoni mwa mwaka, na serikali ya CCK itachangia ujenzi wa nyumba hiyo, hata kama ni ya chumba kimoja.
“CCK tuna sera na ilani nzuri kuliko vyama vyote vya siasa. Hata nyinyi waandishi wa habari tutahakikisha mnapata mazingira bora,” amesema Mwaijojele.
Ameongeza kuwa pamoja na sera hiyo, vipaumbele vyao vinajumuisha elimu, afya, na kilimo, ambavyo vitajadiliwa kwa kina mara baada ya kupata ridhaa ya kugombea nafasi hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED