Rwamugira: Serikali ya TLP itaipa kipaumbele ajira, elimu bure na ulinzi

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 02:41 PM Aug 11 2025

Mgombea urais kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira.
Picha:Ibrahim Joseph
Mgombea urais kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira.

Mgombea urais kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira, amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza taifa, vipaumbele vya serikali yake vitakuwa kuimarisha ulinzi na usalama, kutoa elimu bure, na kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana.

Rwamugira, ambaye ameambatana na mgombea mwenza wake Amana Suleiman Mzee, amesema changamoto ya ajira kwa vijana imekuwa kubwa, hivyo TLP imelenga kuimarisha uchumi ili kutoa nafasi nyingi za ajira.

“Kuna vijana wengi waliomaliza vyuo vikuu na vya kati, lakini wako mtaani bila ajira. Sisi TLP tunakwenda kuimaliza changamoto hiyo,” amesema Rwamugira.

Ameongeza kuwa serikali ya TLP itaimarisha ulinzi na usalama ili kuhakikisha jamii inafanya kazi kwa uhuru na amani.

Kuhusu elimu, amesema chama hicho kitajikita zaidi katika elimu ya ufundi stadi kuanzia ngazi za awali, ili kumpa mwanafunzi ujuzi utakaomsaidia kujiajiri baadaye. Hatua hiyo inalenga kupunguza idadi ya vijana wanaotafuta ajira bila mafanikio.

Aidha, kwa upande wa afya, Rwamugira amesema wataanzisha Bima ya Afya kwa Wote, itakayowawezesha wananchi kupata matibabu pale watakapokabiliwa na changamoto za kiafya.

1