UPEPO wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 unaendelea kuvuma kwa kasi nchini, huku wagombea wa nafasi ya urais na vyama mbalimbali vya siasa vikiendelea kuchukua fomu, kuzindua sera na kusajili wanachama wapya.
Siku zinavyozidi kusonga, ndivyo mchakato wa kidemokrasia unavyochukua sura ya ushindani wa hoja, matumaini mapya na mwelekeo wa mustakabali wa taifa.
Mpaka sasa, jumla ya wanawake wawili wamejitokeza kuwania nafasi ya juu ya urais, huku wengine saba wakigombea nafasi ya makamu wa rais, hatua inayoashiria dalili nzuri za ushiriki wa kijinsia katika siasa.
UCHUMI WA MAJIMBO
Mwajuma Mirambo, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), amejitokeza kuchukua fomu akiahidi mageuzi ya kiuchumi kupitia mfumo shirikishi na kuimarisha majimbo kama vitovu vya maendeleo.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma jana, Mwajuma alisema:
"Kila Mtanzania atanufaika na rasilimali zilizomo katika jimbo lake. Tunalenga uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa kupitia nguvu ya majimbo."
Mwajuma alisema chama chake kitaendeleza ajenda ya maendeleo ya wananchi kwa msingi wa usawa wa fursa, afya bora na utoaji elimu ya msingi hadi juu.
MAPINDUZI YA FIKRA
Georges Bussungu, mgombea wa Chama cha ADA-TADEA, naye alichukua fomu jana huku akiahidi kuleta "mapinduzi ya fikra" na kuimarisha uchumi wa kisasa kupitia teknolojia.
Akisindikizwa na ngoma ya Kigogo na wapambe wake, Bussungu alisema: "Tunahitaji mapinduzi ya njano – yaani mabadiliko ya fikra za taifa zima. Tukiwainua vijana kielimu na kiteknolojia, tunaiokoa Tanzania ya kesho."
ELIMU BURE, AJIRA
Kwa upande wake, Yustas Rwamugira wa Tanzania Labour Party (TLP), alisema endapo atapewa ridhaa na wananchi, serikali yake itahakikisha elimu bure, ulinzi na usalama na kushughulikia changamoto ya ajira kwa vijana.
"Vijana wengi wanaomaliza vyuo hawana ajira. TLP itajikita kwenye elimu ya ufundi na kuimarisha sekta binafsi ili kuongeza nafasi za kazi," alisema Rwamugira ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake, Amana Suleiman Mzee.
Pia alisema serikali yao itaanzisha Bima ya Afya kwa Wote na kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara na uwekezaji wa ndani.
WANACHAMA WAPYA
Wakati wagombea wakichukua fomu, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimeendelea kuvutia wanachama kutoka vyama vingine, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Miongoni mwa waliohamia CHAUMMA ni Lumola Kahumbi aliyekuwa mwanachama wa CHADEMA, ambaye alisema jana kuwa ameamua kuhama kutokana na msimamo wa CHADEMA wa kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
"Msimamo wa 'No Reforms No Election' unawazuia vijana wenye ndoto ya kushiriki uchaguzi. Siasa haiwezi kungoja milele," alisema Lumola, ambaye alitangaza pia nia ya kugombea ubunge wa Bukene kupitia CHAUMMA.
Katika kongamano la vijana lililofanyika Morogoro, Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA Bara, Benson Kigaila, aliahidi mapinduzi kwenye kilimo, ajira kwa vijana, elimu bora na mikopo isiyo na riba kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
UDP YATEUA
Chama cha United Democratic Party (UDP), kimemteua Swaumu Rashidi kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, huku Juma Faki akitajwa kuwa mgombea mwenza, na kwa upande wa Zanzibar, Naymah Salimu atapeperusha bendera ya chama hicho.
Swaumu alipata kura 376 kati ya 390 na kuahidi kuongoza kwa misingi ya amani, upendo na maendeleo katika sekta za kilimo, afya, miundombinu na huduma za jamii.
"Amani na upendo ndio msingi wa kila maendeleo. UDP itakuwa sauti ya walio kimya na itasimamia maslahi ya wananchi," alisema mgombea huyo.
Mwenyekiti wa chama hicho, John Cheyo, alisisitiza kuwa UDP itaendelea kuwa daraja la demokrasia ya kweli na amani.
"Vyama si uadui, bali ni mashindano ya sera na hoja. Hakuna nafasi ya vitisho au chuki. Tuwe wamoja kwa ajili ya Tanzania," alisema Cheyo.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alipongeza UDP kwa maandalizi bora ya mchakato wa uchaguzi na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria na demokrasia.
WALIOCHUKUA FOMU
Mbali na waliojitokeza jana, mpaka sasa wagombea waliochukua fomu za kuomba uteuzi wa INEC kuwania urais mwaka huu ni: Samia Suluhu Hassan (CCM), Coaster Kibonde (MAKINI), Doyo Hassan Doyo (NLD), Kunje Ngombare Mwiru (AAFP), Hassan Almas (NRA) na Twalib Kadege (UPDP).
Pamoja na kusisimka kwa ulingo wa kisiasa, matumaini ya wananchi yameelekezwa kwa wagombea hao kutoa mwelekeo mpya wenye majibu ya changamoto za ajira, afya, elimu na ustawi wa taifa.
Uchaguzi wa mwaka huu unaonekana kuwa wa kihistoria si tu kwa sababu ya idadi ya wagombea, bali pia kwa sura mpya zinazojitokeza, hasa wanawake kuwania nafasi za juu kabisa za uongozi.
Kikwazo kikuu kwa uchaguzi wa mwaka huu kinachotajwa na wataalamu wa sayansi ya siasa, ni kujitoa kwa CHADEMA - chama kikuu cha upinzani nchini.
*Imeandaliwa na Renatha Msungu (DODOMA), Elizabeth Zaya na Maulid Mmbaga (DAR) na Christina Haule (MOROGORO).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED