UCHAGUZI 2025: Mpango aonya uchochezi mitandaoni

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 01:12 PM Aug 12 2025
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango
Picha: Mtandao
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, ametoa maelekezo saba kwa Jeshi la Polisi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza haja ya kuimarishwa usalama, utulivu na amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo.

Akizungumza jana katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Dk. Mpango, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, alisema Jeshi la Polisi linapaswa kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi nyingine ili kufanikisha usimamizi wa taarifa za uchaguzi, hasa zile zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii.

"Mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa la kusambaza sera na ilani, pia hutumika kueneza uchochezi, upotoshaji na taarifa za uongo. Hili ni tishio kwa mshikamano wa kitaifa," alionya.

Alitoa onyo kali kwa makundi au watu wanaopanga kutumia teknolojia, ikiwamo akili unde (AI), kusambaza picha na video za kughushi kwa lengo la kuchafua wagombea au kupandikiza taharuki.

DORIA MITANDAONI

Dk. Mpango aliagiza Jeshi la Polisi kufanya doria mtandaoni (cyber surveillance) kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kubaini, kuchambua na kuchukua hatua haraka dhidi ya taarifa au maudhui yoyote yenye viashiria vya uvunjifu wa sheria.

Pia alisema serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha ununuzi wa helikopta mpya, pamoja na vifaa vya kisasa vitakavyotumika katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

Akisisitiza kaulimbiu ya mkutano huo: "Amani, Utulivu na Usalama Kabla, Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 ni Jukumu Letu Sote", Dk. Mpango alihimiza wananchi, vyama vya siasa na viongozi wa kisiasa kuepuka kujichukulia sheria mkononi pindi wanapoona ukiukwaji sheria za uchaguzi.

Alitaja maeneo saba ambayo Jeshi la Polisi linapaswa kuyasimamia kwa weledi, yakijumuisha ulinzi wa mikutano ya kampeni katika maeneo yaliyopangwa, kudhibiti maandamano yasiyo halali na kuhakikisha wagombea wote wanalindwa bila ubaguzi wa kisiasa.

Mengine ni kudhibiti misongamano inayoweza kuhatarisha maisha, kuzuia vitendo vya rushwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kuhakikisha sheria ya uchaguzi inatekelezwa ipasavyo na kutoa elimu kwa maofisa na askari ili kuongeza uadilifu na utayari.

Alisisitiza ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, hususan katika ngazi za vijiji, mitaa na shehia, kwa lengo la kufanikisha ulinzi jumuishi unaozingatia ushirikishwaji wa jamii.

Dk. Mpango alisisitiza kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa huru, haki na salama, akionya kuwa taasisi yoyote itakayokwamisha azma hiyo itawajibika kwa mujibu wa sheria.

"Lazima wote tuchukue jukumu la kulinda amani yetu. Uchaguzi si uwanja wa vita, bali ni fursa ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka kwa uhuru, bila shinikizo wala hila," alihitimisha.

ANGALIZO LA IGP

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillius Wambura, alibainisha kuwa tayari kuna baadhi ya vikundi vya watu, wanasiasa na wanaharakati walioanza kutoa matamko ya uchochezi yenye lengo la kuvuruga amani ya nchi.

"Tumefanya tathmini ya utekelezaji wetu wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana, na sasa tunapanga mikakati ya kuhakikisha Uchaguzi Mkuu ujao unafanyika kwa amani," alisema IGP Wambura.

Aliahidi kuwa Jeshi la Polisi litachukua hatua kwa wote watakaojaribu kuhatarisha amani kupitia maneno au vitendo vya uchochezi, rushwa ya kisiasa au hujuma za kimtandao.