"Nikipata urais kila mwananchi atafaidika na miradi ya jimbo"- Mwajuma Mirambo

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 02:23 PM Aug 11 2025
Mgombea kiti cha Urais kupitia Chama cha Union for Maltiparty  Democracy (UMD) Mwajuma Mirambo.
Picha:Ibrahim Joseph
Mgombea kiti cha Urais kupitia Chama cha Union for Maltiparty Democracy (UMD) Mwajuma Mirambo.

Mgombea urais kupitia chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Noty Mirambo, amesema sera za chama hicho zimejikita katika uchumi wa majimbo, ili kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na vitega uchumi na miradi iliyopo katika maeneo wanayoishi.

Mirambo alitoa kauli hiyo leo mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma.

Akiwasili takribani saa 5:00 asubuhi katika ofisi hizo, Mirambo amesema sera za UMD ni wezeshi na zinalenga kuinua uchumi wa kila mwananchi mmoja mmoja kupitia rasilimali na fursa zilizopo katika majimbo yao.

“Namshukuru Mungu kwa kukamilisha zoezi hili, ambalo ni hitaji la kikatiba — haki ya kupiga kura au kupigiwa kura. Sisi UMD sasa tuko tayari kuanza michakato ya uchaguzi, na kazi imeanza leo,” amesema Mirambo.

Ameongeza kuwa chama chake kinaamini katika mfumo wa shirikisho wa kuendesha nchi, na kwamba UMD itaunda majimbo yatakayowezesha kila Mtanzania kushiriki moja kwa moja katika kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.