SMZ kuimarisha programu ya makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:08 AM Aug 12 2025
Waandishi wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Picha: Sabato Kasika
Waandishi wakiwa kwenye mafunzo hayo.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeamua kuongeza nguvu katika Programu ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) ili kusaidia kuwa na jamii yenye afya bora.

Akizungumza katika mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari kutoka Zanzibar jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdallah Said, amesema utafiti umeonesha kuwa asilimia 18.6 ya watoto wamedumaa.

“Hivyo, SMZ imeamua kuja na mbinu mpya katika makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto. Programu ya ECD ipo tangu zamani, lakini kwa sasa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameamua programu hii iwe chini ya Taasisi ya Ofisi ya Rais – Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (PDB) kama msimamizi mkuu, kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, na Wizara ya Afya,” alisema Khamis.

Alisema ili serikali iweze kupanga maendeleo, ni muhimu iwe na jamii yenye afya bora. Ameeleza kuwa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yataleta mabadiliko katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe, chanjo, mtoto kunyonyeshwa miezi sita mfululizo bila kupewa chakula kingine, na kutoa elimu ili kupunguza udumavu wa watoto pamoja na vifo.

“Kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, Tanzania imejipanga kuwa nchi yenye uchumi wa kati wa kiwango cha juu. Ili kufikia malengo hayo, tumeamua kufanya mambo makubwa ikiwemo uwekezaji wa dhati katika miundombinu na rasilimali watu. Hatua ya kuwekeza katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto itasaidia kujenga misingi ya akili, maadili na uwezo wa uzalishaji unaohitajika katika uchumi wa kisasa,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali inafanya juhudi za makusudi kuhakikisha watoto wote wanapata huduma bora za afya, lishe, elimu ya awali, na mazingira salama. Ameitaka pia jamii kutambua umuhimu wa ECD, akisisitiza kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo chanya kupitia kalamu zao.

Mtaalamu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kutoka Taasisi ya Children Grassfire, Devis Gisuka, alisema malezi na makuzi ya mtoto huanza tangu akiwa tumboni mwa mama hadi kufikia umri wa miaka minane, ikiwemo mawasiliano na lishe bora.

Mwezeshaji kutoka Madrasa Childhood, Sharifa Suleiman Majid, alisema miongoni mwa mambo yanayochangia mfumo bora wa makuzi ya mtoto ni pamoja na afya bora, lishe, elimu ya mapema, malezi yenye uwajibikaji, ulinzi na usalama wa mtoto.

Mtaalamu wa malezi na makuzi ya awali ya mtoto kutoka UNICEF, Alinune Njemwa, alisema shirika hilo litaendelea kuisaidia Tanzania katika mambo matatu muhimu ili mtoto akue katika ukamilifu wake: kuhakikisha mifumo yote ya ECD inafanya kazi ipasavyo, kusimamia mifumo ya sheria na kanuni katika huduma za malezi, na kuhakikisha jamii, wazazi na walezi wanatoa huduma bora.

Viongozi na waandishi wakiwa katika picha ya pamoja baada kumaliza mafunzo.