Mgombea urais kupitia Chama cha ADA-TADEA, Georges Bussungu, amekuwa mgombea wa saba kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). Bussungu amesema, endapo atachaguliwa, ataongoza mabadiliko ya fikra na kuanzisha mapinduzi katika teknolojia na uchumi wa nchi.
Bussungu amewasili katika viwanja vya Tume majira ya saa 2:50 asubuhi, akiwa ameongozana na mgombea mwenza Ali Makame Issa na wapambe waliokuwa wakicheza ngoma ya kigogo, wakimsindikiza kwa shamrashamra.
Hadi sasa, wagombea wengine waliokwisha kuchukua fomu ni Samia Suluhu Hassan (CCM), Coaster Kibonde (Chama Makini), Doyo Hassan Doyo (NLD), Kunje Ngombare Mwiru (AAFP), Hassan Almas (NRA) na Twalib Kadege (UPDP).
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Bussungu amesema anataka kuleta mtazamo wa usawa katika jamii na mabadiliko yenye manufaa kwa Watanzania, akisisitiza matumizi ya akili mnemba katika kuendesha taifa.
“Chama chetu kinakwenda kuleta mabadiliko makubwa ya fikra, mapinduzi ya teknolojia na uchumi, na mapinduzi ya njano katika fikra za wananchi,” amesema Bussungu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED