CCM kuchangisha bil. 100/- za kampeni

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 12:59 PM Aug 12 2025
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akizungumza na wahariri na waandishi waandamizi wa vyombo vya habari katika Ofisi Ndogo ya CCM Makao Makuu, Lumumba, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: CCM
Picha: CCM
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akizungumza na wahariri na waandishi waandamizi wa vyombo vya habari katika Ofisi Ndogo ya CCM Makao Makuu, Lumumba, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: CCM

ZIKIWA zimebaki wiki mbili kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo kinatarajia kufanya harambee ya kukusanya Sh. bilioni 100 zitakazowezesha kufanikisha mchakato huo.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema harambee hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk. Nchimbi alisema hivi sasa chama kinafanya maandalizi ya kampeni, na kwamba wanahitaji fedha na rasilimali watu ili kufanikisha tukio hilo.

"Sisi tunataka kuonesha mfano wa chama imara kinachowashirikisha wanachama katika maendeleo ya chama chao. Tunatarajia kampeni zichangamke sana, tunataka michango kutoka kwa wanachama ambayo tutaitumia katika kununua tisheti, kofia, kanga fulana na vifaa vingine,” alisema.

Alisema kwa saa 28 kuelekea harambee hiyo CCM inawahimiza wanachama wake na wapenzi kujitokeza kwa wingi kuchangia ili kuonesha nguvu ya chama na nia ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu.

Dk. Nchimbi alisema: "Tukipokea kila aina ya mchango tutaainisha inapotoka. Lakini hatutapokea michango inayodhalilisha utu ama heshima ya taifa. Tutapokea kila aina ya mchango kutoka kwa Watanzania, atakayechangia Sh. 500, Sh. 1,000, Shilingi milioni moja wote tutapokea."

Hata hivyo, aliwakaribisha Watanzania wengine ambao hawana mapenzi na CCM kujitokeza kuchangia.

Alisema kunapofanyika harambee yoyote matarajio huwa ni mawili ambayo ni kufikia lengo au kushindwa, akisema kuelekea harambee hiyo CCM imejapanga kwa matokeo yote mawili na itawashukuru Watanzania kwa yote.

Vilevile, alisema harambee hiyo haitaathiri mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani kwa sababu Kamati ya Maadili ya CCM ya kuchambua tabia ya kila mgombea imeshakaa.

Alisema kuwa watakaochangia kidogo na kikubwa wote wataheshimiwa na kupokea michango yao kwa ajili ya kufanikisha lengo.

Kadhalika, Dk. Nchimbi alisema idadi ya wanachama wa CCM wanaojiandikisha kidijitali inazidi kuongezeka kila siku, na kueleza kuwa hadi kufikia jana asubuhi idadi ilikuwa ni milioni 13.19.