Vijana 400 wazindua Ilani ya Vijana 2025/30 Dar

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 12:44 PM Aug 11 2025
Mwakilishi wa Ajenda ya Vijana, Joseph Malekela
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwakilishi wa Ajenda ya Vijana, Joseph Malekela

Vijana 400 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uzinduzi wa Ilani ya Vijana 2025/2030, yenye lengo la kuongeza ushiriki wa kundi hilo katika maendeleo ya taifa, utawala bora wa kidemokrasia, amani na ustawi wa kijamii.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Agosti 11, 2025, katika Makumbusho ya Taifa, ukiongozwa na Mwakilishi wa Ajenda ya Vijana, Joseph Malekela, ambaye alisema ilani hiyo inabeba matamanio, ndoto na mahitaji ya vijana katika nyanja mbalimbali.

Malekela ametaja nguzo kuu tano za kipaumbele zilizomo kwenye ilani hiyo kuwa ni:

  1. Vijana na Uongozi – kuongeza ushiriki wa vijana katika maamuzi kwenye ngazi zote za serikali na jamii.


  1. Elimu na Teknolojia – kuhakikisha elimu bora, jumuishi na inayolingana na mahitaji ya soko la ajira la karne ya 21, sambamba na upatikanaji wa taarifa sahihi na jumuishi kwa wakati.


  1. Ajira na Fursa za Kiuchumi – kuongeza ajira na kukuza ujasiriamali miongoni mwa vijana.


  1. Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi – kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira.


  1. Afya na Ustawi – kuhakikisha huduma bora za afya na ustawi wa kijamii kwa vijana.

Ameongeza kuwa ilani hiyo inataka kuwepo mkataba wa kijamii kati ya vijana na viongozi, ikiwasihi vyama vya siasa, watunga sera na taasisi kuingiza vipaumbele hivyo katika mipango yao.

Kwa upande wake, Mratibu wa Ajenda ya Vijana, Ocheck Msuya, amesema hatua hiyo inalenga kutoa vipaumbele na matarajio bayana, huku ikizingatia mahitaji ya makundi maalum. Pia alibainisha kuwa ilani hiyo imeandikwa kwa mfumo wa nukta nundu ili kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kuona kuisoma.

Neema Divyele, Katibu wa Watu Wenye Ulemavu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, ameitaka serikali kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu na kuwapa kipaumbele wakati wa kupiga kura.

Naye Elisha Luambano amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya vijana katika nafasi mbalimbali za maamuzi, ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.