SERIKALI imewataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kwenda uwanjani kwa ajili ya kuzishangilia timu nyingine ambazo zinashiriki mashindano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), yanayoendelea nchini, Kenya pamoja na Uganda.
Rai hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ambapo alifunguka kuwa haipendezi uwanja kuwa mtupu pindi timu nyingine mbali na Taifa Stars, zinapocheza.
"Haipendezi kuona uwanja wa Benjamin Mkapa upo wazi timu nyingine zinapocheza, haya ni mashindano yetu wote, ninaomba Watanzania waendelee kujitokeza kwa wingi kwani tiketi zinapatikana," alisema Msigwa.
Alisema Mashindano hayo yameleta faida kubwa za kiuchumi katika taifa letu kwa wageni wengi kuvutiwa na vivutio vyetu.
Aidha, aliipongeza Timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars), kutokana na juhudi kubwa inayoifanya katika mashindano hayo.
Katibu huyo, pia alilipongeza kwa kiasi kikubwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kutokana na hamasa kubwa wanazozifanya kuhakikisha Watanzania wanajitokeza kwa wingi uwanjani.
Alisema uwapo wa hamasa hizo unazidi kuwapa morali wachezaji kupambana kufa kupona ili kuweze kutimiza lengo la kuusaka ubingwa wa michuano hiyo.
Taifa Stars, ambayo tayari imefuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, inaongoza msimamo wa Kundi B, ikiwa na alama tisa kileleni, ikifuatiwa na Mauritania yenye ponti nne, Burkina Faso alama tatu na Madagascar pointi moja huku Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiburuza mkia bila pointi.
Kinara wa Kundi B, atakutana na mshindi wa pili wa Kundi A, lenye timu za Angola, DR Congo, Morocco, Zambia na mwenyeji Kenya, huku mechi hiyo ikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Timu itakayoshika nafasi ya pili katika Kundi B, itakutana na kinara wa Kundi A, na mechi hiyo ikipigwa nchini Uganda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED