Serikali imesema utekelezaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) unapaswa kuzingatia sio tu sheria, kanuni na miongozo ya uratibu, bali pia matakwa ya sheria nyingine za nchi.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaid Ally Hamis, amesema hayo jana jijini Dodoma alipofungua Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
“Ikumbukwe kuwa, uzingatiaji wa misingi ya uwazi na uwajibikaji kupitia sheria, kanuni na miongozo wakati wa utekelezaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ndio msingi wa utambuzi wa mchango wao katika nyanja mbalimbali na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Aidha, amesema ni matumaini ya Serikali kupitia wizara yenye dhamana na mashirika hayo kuwa majadiliano na shughuli zote zinazofanyika sambamba na kongamano hilo la mwaka yataleta tija na matokeo chanya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED