Mwili wa Ndugai wazikwa Kongwa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 12:54 PM Aug 12 2025
Mwili wa Spika Mstaafu na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai ukishushwa kaburini katika mazishi yaliyoanyika katika kijiji cha Msunjulile Kongwa, Mkoani Dodoma, Agosti 11, 2025
Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu
Mwili wa Spika Mstaafu na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai ukishushwa kaburini katika mazishi yaliyoanyika katika kijiji cha Msunjulile Kongwa, Mkoani Dodoma, Agosti 11, 2025

KWA heshima na simanzi kubwa, mwili wa Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Job Yustino Ndugai, umezikwa kijijini kwake Madubwa, kata ya Sejeli, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma.

Mamia ya waombolezaji kutoka kila kona ya nchi walijitokeza jana katika maziko ya kiongozi huyo aliyegusa maisha ya wengi kwa uadilifu, hekima na uongozi wa kipekee.

Ibada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Maimbo Mndolwa, ilifanyika katika Kanisa la Mtakatifu Michael, Dinar ya Kongwa. 

Akihubiri mbele ya waombolezaji, Dk. Mndolwa alisema taifa limepoteza mtu aliyekuwa na vipawa vingi vilivyotumika kwa ustawi wa jamii, kanisa na nchi kwa ujumla.

"Alikuwa na ulimi mnono uliojaa busara. Kauli zake hazikuwa za kubahatisha. Alisimama na kusema yaliyo ya kweli. Hakika alipewa karama ya pekee na Mungu, na aliitumia kuleta amani, ushawishi na utulivu," alieleza askofu huyo.

Aliongeza kuwa Hayati Ndugai alitumika vyema si tu kama mzee wa kanisa, bali hata alipoinuliwa kuwa mshauri wa maaskofu, kutokana na mwenendo wake wa maisha na hekima aliyonayo.

Katika ujumbe wake mzito, Askofu Mndolwa aliwataka viongozi na wananchi kutafakari kuhusu matumizi ya vipawa walivyopewa, akisisitiza:

"Ndugai ametimiza wajibu wake, lakini sisi tuliobaki tunajiuliza 'tunaifanyia nini karama yetu? Wapo waliopewa fedha, uongozi, ushauri, au ulezi lakini wanavitumia vibaya. Tuige mfano wa mtumwa mwema kama Job Ndugai."

AHADI YA SERIKALI

Mara baada ya maziko, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza kwa niaba ya serikali, alisisitiza kuwa miradi na maono ya Hayati Ndugai havitaachwa kufifia.

"Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kukamilishwa kwa masuala yote aliyoyaacha. Tutahakikisha Kongwa inatangazwa rasmi kuwa sehemu ya kihistoria ya harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika," alisema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu alieleza kuwa Hayati Ndugai alikuwa kiunganishi thabiti kati ya Bunge na serikali, na mchango wake umeacha alama kubwa katika ustawi wa siasa na maendeleo ya taifa.

"Alikuwa mwanamageuzi, mzalendo, mchapakazi, na kiongozi aliyeiweka Kongwa katika ramani ya maendeleo. Ameondoka, lakini alama zake ni hai – ndani ya Bunge, ndani ya kanisa, na ndani ya mioyo ya Watanzania," alisema Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

WASIFU WA HESHIMA

Wasifu wa Hayati Ndugai ulisomwa kwa hisia na heshima, ukionesha maisha yake kama mwanafunzi, mwalimu, mwanasiasa, kiongozi wa Bunge, mfuasi mwaminifu wa kanisa na baba wa familia. Alitajwa kuwa mtu wa watu, aliyetoa kwa moyo, aliyechukia ubaguzi na aliyependa haki.

Katika sala ya mwisho, waombolezaji waliombwa kuiga moyo wa kujitoa wa Hayati Ndugai, wakikumbushwa kuwa kifo chake si mwisho, bali mwaliko wa kutafakari maisha ya mwanadamu na jinsi anavyotumikia taifa na jamii.