SIKU YA VIJANA; Mitandao ya kijamii ilivyo fursa, maangamizi na tumaini la taifa

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 01:05 PM Aug 12 2025
Simu janja
Picha; Mtandao
Simu janja

KATIKA kila jamii, vijana ni nguzo imara inayotegemewa leo na kuaminiwa kesho. Wakiwa na nguvu, ari, ndoto na ubunifu wa hali ya juu, vijana ndio injini ya maendeleo ya taifa.

Hata hivyo, licha ya umuhimu wao, kundi hili linakumbwa na mawimbi ya changamoto nyingi katika dunia ya kisasa iliyojaa kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia, hasa mitandao ya kijamii. 

Mitandao ya kijamii kama TikTok, Instagram, Facebook, WhatsApp, na X (zamani Twitter), imebadilisha namna vijana wanavyowasiliana, kujifunza, kufanya biashara, kuhamasisha jamii na hata kujitambulisha. 

Lakini kama ilivyo kwa kisu chenye makali pande zote mbili, mitandao hii imekuwa pia chanzo cha changamoto kubwa kwa maisha yao.

IDADI KUBWA

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania ina vijana zaidi ya milioni 21, sawa na asilimia 34.5 ya watu wote. Kati yao, asilimia 21.7 wanafanya kazi zisizohitaji ujuzi maalum, jambo linaloonesha changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira rasmi.

Rehema Nassor, kijana mwenye umri wa miaka 24 anayetumia mitandao kama jukwaa la kutangaza biashara ya vipodozi, anasema:

"Vijana wengi, hata waliomaliza vyuo vikuu, wapo mitaani bila kazi. Wengine hukata tamaa, kujiingiza katika biashara haramu au uhalifu. Hili linapaswa kutazamwa kwa jicho pana."

Na si ajira tu. Matumizi mabaya ya mitandao pia yamesababisha matatizo ya afya ya akili, mmomonyoko wa maadili, na ongezeko la tabia hatarishi miongoni mwa vijana.

ATHARI ZINAZOUMIZA

Takwimu kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) zinaonesha hali ya kutisha: zaidi ya watu 900,000 walitibiwa uraibu wa dawa za kulevya mwaka 2023. Kati yao, vijana ndio kundi linaloathirika zaidi, huku Dar es Salaam ikiongoza kwa kuwa na zaidi ya waraibu 230,000.

Rehema anaeleza kuwa shinikizo la kufanikiwa haraka linaathiri sana vijana wa kizazi hiki. "Mitandao imekuwa kioo cha maisha ya kifahari. Kila mtu anataka kuonekana anaishi kama ‘mastar’. Matokeo yake ni msongo wa mawazo, huzuni, na hata visa vya kujiua," anaeleza kwa uchungu.

Vilevile, Rehema anataja mmomonyoko wa maadili kuwa tishio lingine linalochochewa na mitandao. 

"Baadhi ya vijana huacha mila na desturi zetu kwa kushawishika na maisha ya kigeni, wakijikuta kwenye tabia hatarishi kama zinaa, utapeli na lugha chafu," anabainisha.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Machi 2025 inaonesha Tanzania ina laini za simu zaidi ya milioni 90, huku watumiaji wa intaneti wakifikia milioni 49.3 sawa na asilimia 72 ya Watanzania. Simu janja zinazotumia teknolojia ya kasi (5G) ni asilimia 23, huku 4G ikiongoza kwa asilimia 91.

Hii ni picha ya taifa lenye matumizi makubwa ya teknolojia, lakini swali ni: je, vijana wanaitumia kwa tija?

Ingawa changamoto zipo, mitandao ya kijamii pia imefungua milango ya fursa lukuki kwa vijana. Rehema anathibitisha: "Kupitia mitandao, nimejifunza mbinu za biashara, kupata wateja na kujiingizia kipato. Sihitaji ofisi wala duka, simu yangu ni biashara."

Catherine Mathayo (32), mwalimu kwa taaluma, anaunga mkono: "Mitandao imerahisisha mawasiliano ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Vijana sasa wanaweza kuongoza kampeni dhidi ya ukatili, rushwa, au mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia simu."

Anasisitiza vijana wanaweza kujifunza kupitia kozi za mtandaoni, kusoma makala za ujasiriamali, au kupata fursa za ufadhili wa masomo nje ya nchi. Lakini si wote wanaotumia kwa namna hiyo.

"Kama unatumia kifurushi cha Sh. 10,000 kuperuzi umbea na siyo maarifa, unapoteza muda na maisha yako," anatahadharisha.

Catherine anaeleza kuwa baadhi ya vijana wameathiriwa na picha za maisha ya kifahari wanazoziona mitandaoni. 

"Wanajilinganisha na wengine, wakidhani kila mtu anayeishi maisha mazuri ni ya kweli. Hii hupelekea wivu, sonona, au hata uamuzi mbaya," anasema.

Anaongeza kuwa baadhi ya vijana wameathiriwa na unyanyasaji mtandaoni: matusi, kejeli au hata video za aibu kusambazwa bila idhini yao. Wengine huingia katika uhusiano ya kitapeli au kuibiwa na matapeli.

Kwa mujibu wa ripoti ya TCRA, mikoa ya Rukwa na Morogoro inaongoza kwa matukio ya ulaghai wa mtandaoni. Wilaya kama Sumbawanga, Ifakara na Kilombero zina idadi kubwa ya visa vya udanganyifu huu.

HATUA ZA KISHERIA 

Serikali nayo haijalala. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, alieleza Aprili 2025 kuwa sheria zinazosimamia michezo ya kubahatisha zinafanyiwa marekebisho, kwani baadhi zimegeuka kuwa "janga la kitaifa," hasa kwa vijana wanaoshiriki kamari ya mtandaoni.

Kwa upande wake, Catherine anasema elimu kuhusu matumizi salama ya mitandao ni muhimu zaidi sasa. "Shule, vyuo na taasisi za dini zinapaswa kuwa mstari wa mbele kuwapa vijana elimu ya stadi za maisha na matumizi salama ya teknolojia."

Julai 2025, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo alitangaza kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inalenga kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuhakikisha kuna usawa wa kiuchumi. 

Hii ni hatua ya msingi kuhakikisha vijana wanajumuishwa kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Catherine anashauri: Wazazi wasiwe mbali na watoto wao: wawasikilize, waelekeze, na wawe sehemu ya maisha yao.

Serikali ianzishe vituo vya msaada wa kisaikolojia shuleni na vyuoni, vijana wapewe nafasi kwenye vyombo vya uamuzi ili wajisikie kuwa sehemu ya taifa, si walalamikaji tu mitandaoni na sekta binafsi na serikali zishirikiane kutoa mikopo na mafunzo kwa vijana walio tayari kujiajiri.

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, Toleo la 2024, inatambua mchango wa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35. Inasisitiza umuhimu wa kuwajengea vijana ujuzi, maadili, na uwezo wa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Sera hii inaelekeza pia kuimarishwa kwa programu za elimu ya kidijitali, hasa vijijini, ili kuhakikisha vijana wote wanapata fursa sawa za kujifunza na kunufaika na teknolojia.