Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimetangaza dhamira yake ya kukipeleka Chama Cha Mapinduzi (CCM) “likizo isiyo na muda wa kumalizika” kwa kuongoza nchi kupitia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza katika kongamano la vijana mkoani Morogoro, Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA Bara, Benson Kigaila, amesema chama hicho kitaongoza kwa kuzingatia sera tatu kuu.
Sera ya kwanza ni kuhakikisha vijana wanaomaliza shule na vyuo wanapata ajira, kwa kuimarisha mifumo ya kilimo cha umwagiliaji na kuacha utegemezi wa mvua, sambamba na kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika mazao.
Sera ya pili ni kuimarisha mikopo isiyo na riba kupitia Halmashauri kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Kigaila alisema hatua hiyo itawaepusha wanawake na mikopo yenye masharti kandamizi maarufu kama “mikopo ya kausha damu.”
Sera ya tatu inalenga kuboresha shule za Serikali kuanzia msingi hadi vyuo vikuu ili ziwe bora kuliko shule binafsi. Uboreshaji huo utahusisha upatikanaji wa walimu wa kutosha, madarasa, vyoo, madawati na vitabu vya kujifunzia na kufundishia, ili kuhakikisha watoto kutoka familia masikini wanapata elimu bora bila kutegemea shule binafsi.
Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya Vijana Taifa wa CHAUMMA, Nkola Abubakar, alikitaka chama hicho kuanzisha jukwaa la elimu ya uraia na siasa kwa vijana mara kwa mara, pamoja na kuhakikisha vijana wengi wanapewa nafasi za kugombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili kupata viongozi vijana kwa mustakabali wa baadaye.
Naye Mkurugenzi wa Tafiti, Operesheni na Ufuatiliaji wa CHAUMMA Taifa, Elia Evarist, aliitaka jamii kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo wa Oktoba, akisema ni njia pekee ya kudai haki na kupinga dhuluma wanazokabiliana nazo, ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED