Miaka mitano ya kuisuka Muhimbili mpya kwa trilioni 1.2/-

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:54 PM Mar 06 2025
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji MNH Dk. Rachel Mhaville
Picha: MNH
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji MNH Dk. Rachel Mhaville

SERIKALI imetenga Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa kuijenga upya ili kuwezesha huduma zote kutolewa ndani ya jengo moja litakalokuwa na vitanda 1,757 kutoka vitanda 1,435 vya sasa.

Kati ya fedha hizo dola milioni 364 zitatoka Korea Kusini na Serikali ya Tanzania itachangia dola za milioni 104. 

Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dk. Rachel Mhaville, amesema hayo leo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi.

Alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya mafanikio ya kipindi cha miaka minne chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, na kwamba upembuzi yakinifu wa mradi huo, umekamilika.Amesema utekelezaji wa mradi huo ni wa awamu moja, ambao utachukua miaka mitano kukamilika baada ya kusaini mkataba, hatua hii haitaathiri utoaji wa huduma hospitalini hapa hivyo huduma zitaendelea kutolewa kama kawaida.

“Utekelezaji wa mradi huu wa kihistoria katika sekta ya afya nchini na Ukanda wa Afrika, utakuwa na faida lukuki ikiwamo kuboreshwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kupitia vifaa tiba vya kisasa. “Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, kuwezesha wagonjwa kupata huduma zote katika eneo moja, kupunguza mizunguko na usumbufu pamoja na kuwa na mpangilio mpya wa hospitali huku eneo kubwa likibaki wazi kwa matumizi ya maendeleo mengine miaka 50 ijayo,” amesema Dk. Mhaville.

MNH, yenye kampasi mbili ni Hospitali ya Rufani ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini, ina vitanda 2,043 ambapo Upanga kuna vitanda 1,435 na Mloganzila vipo 608.

Katika kampasi zote mbili wagonjwa 4,000 wanaonwa kwa siku.